Hizbullah: Wananchi wa Lebanon hawatobadilika kwa sababu ya vikwazo vya Marekani
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, siasa za vikwazo za Marekani haziwezi kuwafanya wananchi wa Lebanon walegeze kamba na kubadilisha msimamo wao.
Sheikh Naim Qassim amezungumzia tamko la serikali ya Marekani la kuiwekea vikwazo Lebananon na kueleza kwamba, vikwazo hivyo haviwezi kuwa na taathira kwa wananchi wa Lebanon katika msimamo wao bali hilo litawafanya wazidi kusimama kidete na kushikmana zaidi na muqawama na mapambano.
Baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kupata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri katika eneo la Asia Magharibi, Marekani imeshadidisha njama na mashinikizo yake dhidi ya harakati hiyo, ambapo benki na shakhsia ambao wana mfungamano na harakati hiyo wamewekwa katika orodha ya ya vikwazo ya serikali ya Washington.
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria matukio ya Lebanon hasa kuundwa serikali mpya nchini humo na kueleza kwamba, Hizbullah itakuwa pamoja na serikali ambayo imeundwa kutokana na akthari ya mirengo na makundi ya kisiasa ya nchi hiyo.
Rais Michel Aoun wa Lebanon tarehe 31 ya mwezi uliopita wa Agosti alimteua Mustapha Adib kuwa Waziri Mkuu na kumpa jukumu la kuunda serikali mpya baada ya kujiuzulu serikali iliyokuwa ikiongozwa na Hassan Diab.