Mahakama ya Yemen yawahukumu kifo Trump na Bin Salman
Mahakama ya Jinai katika mkoa wa Saada nchini Yemen imewahukumu kifo watu kumi wakiwemo Rais wa Marekani, Donald Trump na mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman kwa kuhusika na shambulizi lililolenga basi la wanafunzi na kuua makumi miongoni mwao mwaka 2018.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Saba, mahakama hiyo imepasisha hukumu ya kifo kwa watu hao baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya wanafunzi 51 wa Dhahyan katika hujuma iliyolenga basi lao la skuli. Shambulizi hilo la kikatili la mwaka 2018 lilifanywa na ndege za kivita za muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Jaji mkuu wa mahakama hiyo, Riyadh al-Ruzami amesema mbali na Trump na Bin Salman, wengine wanaopaswa kunyongwa kwa mujibu wa hukumu hiyo ni Turki bin Bandar bin Abdulaziz al-Saud, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Norman Mattis na Giselle Norton Allen Schwartz.
Wengine ni rais mtoro wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbilia Saudia, Abd Rabb Mansour Hadi, Ali Mohsen Saleh al-Ahmar, Ahmed Obaid Bin Dagher na Mohammad Ali Ahmad al-Maqdashi.
Kadhalika mahakama hiyo ya jinai katika mkoa wa Saada nchini Yemen imewataka kumi hao waliopatikana na hatia walipe fidia ya dola bilioni 10 kwa familia za watu waliouawa katika shambulizi hilo dhidi ya basi la shule.
Kwa mujibu wa shirika la utafiti la Armed Conflict Location and Event Data Project (ACLED), Wayemen 56,000 wameuawa katika mashambulizi yanayofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Riyadh dhidi ya Wayemen tokea Machi mwaka 2015.