Faisal Mekdad: Askari wa Marekani wanapaswa kuondoka Syria
Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Syria amesema kuwa magaidi ndio wenzo wa bei rahisi zaidi unaotumiwa na Marekani katika kanda ya magharibi mwa Asia na kwamba askari wa Marekani wanapaswa kuondoka katika ardhi ya Syria.
Faisal Mekdad aliyasema hayo jana katika mahojiano yake na gazeti la al Watan akiashiria harakati za Wamarekani kwa ajili ya kupanua zaidi sera zao za kuwahujumu wananchi wa Syria kisiasa na kijeshi. Amesema kuwa, Washington inaendeleza sera zake za kuwahujumu na kuwashambulia Wasyria kisiasa na kijeshi na inayatumia makundi ya kigaidi kutekeleza sera hizo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameongeza kuwa, Syria yenye umoja na mshikamano inaweza kukabiliana na njama za Marekani zinazofanyika kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Faisal Mekdad amesisitiza kuwa Wamarekani wanapaswa kuondoka katika ardhi ya Syria bila ya masharti yoyote, na sambamba na hayo Wasyria wanapaswa kuzidisha juhudi za kitaifa za kuimarisha amani na usalama.
Marekani imetuma maelfu ya wanajeshi huko kaskazini mwa Syria kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi bila ya ridhaa wala ruhusa ya serikali ya Damascus. Hii ni licha ya kuwa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Saudi Arabia na washirika wao wengine ndio wafadhili wakuu wa makundi ya kigaidi yanayopigana dhidi ya serikali halali ya Syria.