Assad aikosoa Saudi Arabia kwa kushirikiana na magaidi nchini Syria
(last modified Tue, 06 Oct 2020 11:18:27 GMT )
Oct 06, 2020 11:18 UTC
  • Rais Bashar Assad wa Syria
    Rais Bashar Assad wa Syria

Rais Bashar Assad wa Syria amesema kuwa misaada na himaya kubwa ya Saudi Arabia kwa makundi ya kigaidi ndiyo sababu kuu iliyoliwezesha kundi la kigaidi la Daesh kuteka na kukalia kwa mabavu maeneo ya nchi hiyo mwaka 2014.

Bashar Assad amesema kuwa mwaka 2014 Saudi Arabia ikishirikiana na Qatar, Marekani, Uingereza na Ufaransa iliyasaidia na kuyafadhili makundi ya kigaidi ya kuyawezeha kutwaa maeneo ya ardhi ya nchi hiyo sambamba na kusababisha hasara kubwa za mali na nafsi kwa wananchi wa Syria. 

Wakati huo huo mshauri wa masuala ya kisiasa na vyombo vya habari wa Rais wa Syria, Bouthaina Shaaban amesema kuwa magaidi waliingizwa Syria na Uturuki kwa msaada wa fedha za Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Lengo la vita vya Saudia huko Yemen pia ni kuuza silaha za Israel na kuyapa faida kubwa makampuni ya kutengeza silaha.

Bouthaina Shaaban

Shaaban amemkosoa pia Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki na kusema: Erdogan anafanyakazi ileile aliyoifanya Syria katika mgogoro wa Nagorno-Karabakh kwa kusimama pamoja na Azerbaijan dhidi ya nchi ya Armenia.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa hujuma kubw ya makundi ya kigaidi yaliyokuwa yakifadhiliwa na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao. Hata hivyo jeshi la Syria limefanikiwa kuzima hujuma hiyo na kuwafurusha magaidi hao katika sehemu kubwa ya nchi hiyo kwa msaada na himaya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia.