Marekani yaiba tena mafuta ya Syria na kuyapeleka Iraq
Msafara wa malori 20 ya Marekani yaliyobeba mafuta ghafi yaliyoibwa kutoka visima vya mafuta vya Syria umeelekea nchini Iraq.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Syria (SANA), msafara huo wa malori ya Marekani yaliyobeba mafuta ya kuporwa uliondoka jana Jumamosi katika mkoa wa al-Hasakah, kaskazini magharibi mwa Syria na kuelekea Iraq kupitia kivuko haramu cha al-Walid katika eneo la al-Yaroubia.
Katika miezi kadhaa iliyopita, wanajeshi wa Marekani wameonekana wakipora maelfu kwa maelfu ya mapipa ya mafuta ya Syria na kuyaingiza nchini Iraq kwa njia za magendo.
Tokea mwaka 2019, Marekani iliingiza wanajeshi wake katika maeneo ya visima vya mafuta vilivyo katika mikoa ya al-Hasakah na Deir ez-Zor ambayo inadhibitiwa na Wakurdi kaskazini mwa Syria.
Hivi karibuni Wizara ya Ulinzi ya Russia iliashiria wizi wa mafuta ya Syria unaofanywa na Marekani na kutangaza kuwa: Biashara inayofanywa na Marekani ya mafuta ya Syria inaipatia nchi hiyo faida ya dola milioni 30 kwa mwezi.
Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana Donald Trump alisema kuwa, licha ya wanajeshi wa Marekani kuondoka kaskazini mashariki mwa Syria lakini idadi ndogo ya wanajeshi hao itabakia katika maeneo yenye utajiri wa mafuta ya Syria eti kwa shabaha ya kulinda visima vya mafuta vya nchi hiyo.