Imarati yasaini mkataba wa kununua bidhaa zinazotengenezwa katika vitongoji vya Wazayuni
Umoja w Falme za Kiarabu (Imarati) umesaini mkataba mpya wa kununua bidhaa zinazotengenezwa katika vitongoji vya walowezi Kizayuni vilivyojengwa kwenye ardhi walizoporwa Wapalestina za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post leo limeandika kuwa, Kampuni ya FAM Holding ya Imarati itaingiza nchini humo bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya Wazayuni vya Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan kama mafuta ya zaituni, unga wa ngano na asali.
Huko nyuma pia Mohammad Shtayyeh Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina aliitolea mwito jamii ya kimataifa kususia bidhaa zinazotengenezwa katika vitongoji hivyo vya Wazayuni kwani zimezalishwa katika ardhi walizoporwa Wapalestina.
Umoja wa Mataifa, mwezi Februari mwaka huu ulichapisha orodha nyeusi ya majina 112 ya makampuni yanayofanya kazi katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds Mashariki na katika miinuko ya Golan ambapo makampuni 94 yalikuwa ni ya Kizayuni na 18 kutoka katika nchi sita duniani. Makampuni yaliyoko kwenye orodha hiyo nyeusi ni pamoja na mashirika ya kibenki, simu za mkononi, ujenzi na ya sekta mbalimbali za teknolojia.