Palestina yaishtaki rasmi Imarati Umoja wa Mataifa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina Riyadh al Maliki amewasilisha rasmi mashtaka dhidi ya Imarati kwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet.
Gazeti la Al Qudsul-Araby limeripoti kuwa, Mamlaka ya Ndani ya Palestina imeishtaki Imarati Umoja wa Mataifa kwa kukiuka sheria za kimataifa zinazohusu marufuku ya bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Riyadh al Maliki amesisitiza kuwa, mnamo mwaka huu wa 2021, Israel na mashirika yake ya kikoloni na ya kibepari imesaini mikataba ya kibiashara na mashirika kadhaa ya Imarati, makubaliano ambayo yanakiuka "orodha nyeusi" iliyotolewa na ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa inayohusiana na marufuku ya kuamiliana kibiashara na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina amebainisha kuwa, mikataba ya makubaliano iliyoasianiwa baina ya Imarati na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni utangulizi wa kusainiwa mikataba mingine kwa kisingizio cha kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mashirika ya Imarati na vitongoji haramu vya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, hatua ya utawala wa haramu wa Israel ya kuwazuia Wapalestina kuwekeza katika ardhi zao zinazokaliwa na walowezi wa Kizayuni imesababisha hasara ya dola bilioni 3.4 kwa uchumi wa Palestina.
Hivi karibuni na baada ya kusaini mkataba wa mapatano wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, Umoja wa Falme za Kiarabu umesaini mikataba ya kiuchumi na kibiashara na mashirika ya Kizayuni ambayo mengi yao yako kwenye vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi, ikiwemo ya ununuzi wa vileo kutoka kitongoji cha Itmar kilichoko kwenye vijiji vya Aurta, Bait Faurki na Aqraba katika eneo la Nablus.../