Mabilioni ya dola yapotea katika vita vya Marekani huko Afghanistan
Wasimamizi wa serikali ya Marekani wametoa ripoti na kukiri juu ya kupotea mabilioni ya dola fedha zilizotumika katika vita vya miaka 20 vya nchi hiyo huko Afghanistan.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti kuwa, wasimamizi wa serikali ya Marekani leo wametoa taarifa na kueleza kuwa Marekani imepoteza mabilioni ya dola kwa ajili ya majengo na magari huko Afghanistan; vitu ambavyo vimeachwa hivi hivi au vimeharibika. Katika ripoti yao hiyo wasimamizi wa serikali ya Marekani wamechunguza kiasi cha dola bilioni saba na milioni 800 zilizotumika huko Afghanstan na kueleza kuwa ni majengo na vyombo vya usafiri tu vyenye thamani ya dola milioni 343 na laki mbili ambavyo vimehifadhiwa vizuri huko Afghanistan.
Mkaguzi Mkuu Maalumu wa Marekani ametangaza katika ripoti hiyo kuwa, wananchi wa Marekani wamechoshwa na vita vya miaka 20 vilivyoanzishwa na nchi yao huko Afghanistan; na Rais Joe Biden wa Marekani hivi sasa anachunguza makubaliano ya amani yaliyosainiwa mwaka mmoja uliopita kati ya Donald Trump na kundi la Taliban.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa makubaliano hayo; Marekani inapasa kuamua je, itawaondoa huko Afghanistan wanajeshi wake wake wote hadi kufikia tarehe Mosi mwezi Mei au watabaki nchini humo, na je, upo uwezekano wa vita kuendelea kwa muda mrefu?
Marekani na waitifaki wake mwaka 2001 waliivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kudhamini amani nchini humo. Hii ni katika hali ambayo tangu wakati huo hadi sasa hali ya mchafukoge, ukosefu wa amani, ugaidi na uzalishaji wa madawa ya kulevya vimeongezeka pakubwa nchini Afghanistan.