Kwa nini Papa Francis amefanya safari nchini Iraq?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i67616-kwa_nini_papa_francis_amefanya_safari_nchini_iraq
Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani jana alikutana na kufanya mazungumzo mjini Najaf Iraq na Ayatullah Sayyid Ali Sistani Marjaa mkubwa wa Kishia nchini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 07, 2021 12:03 UTC
  • Kwa nini Papa Francis amefanya safari nchini Iraq?

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani jana alikutana na kufanya mazungumzo mjini Najaf Iraq na Ayatullah Sayyid Ali Sistani Marjaa mkubwa wa Kishia nchini humo.

Safari ya Papa imefanyika katika hali hali ambayo, hivi sasa ulimwengu unakabiliwa na janga kubwa la virusi vya Corona na katika mazingira haya ambayo takribani aghalabu ya safari wa kidiplomasia nazo zimesitishwa au zimewekewa mipaka na sheria kali.  Haya ni mambo ambayo, yanaongeza umuhimu wa safari ya Papa Francis nchini Iraq.

Inaonekana kuwa, moja ya sababu za safari ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani nchini Iraq ni hii kwamba, kabla ya hapo viongozi waliotangulia wa Kanisa Katoliki wamewahi kualikwa nchini humo lakini mazingira ya kufanyika safari hizo hayakutimia. Gazeti la Marekani la New York Times limeandika kuhusiana na sababu za safari ya Papa Francis kwamba: Safari kama hii lilikuwa tumaini la miaka kadhaa la Papa. Papa John Paul II mwaka 2000 alitaka kuitembelea Iraq, lakini safari hiyo iliahirishwa baada ya kushadidi mivutano katika eneo la Asia Magharibi.

Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani alipowasili Baghdad na kulakiwa na Mustafa al-Kadhimi, Waziri Mkuu wa Iraq

 

Papa Benedict XVI naye aliwahi kualikwa aitembelee Iraq, lakini kutokana na vita hakuweza kuitikia mwito huo. Rais Barham Salih wa Iraq Julai 2019 alimualika Papa Francis akiwa na matumaini kwamba, hilo litasaidia kuboresha hali ya mambo baada ya miaka mingi ya vuta nikuvute na machafuko katika nchi hiyo ya Kiarabu. Papa Francis aliitikia mwaliko huo na kuitangaza bayana kwamba, hataki kuwakatisha tamaa wananchi wa Iraq hususan jamii ya Wakristo ambayo imeonja machungu ya taabu na masaibu mengi.

Sababu ya pili ya Papa kuichagua Iraq kwa ajili ya kufanya safari wakati huu ni idadi ya Wakristo walioko katika nchi hiyo. Katika miaka ya mwisho ya utawala wa dikteta Saddam idadi ya Wakristo nchini Iraq ilikuwa inafikia milioni 1.5. Hata hivyo idadi hiyo imepungua kwa theluthi moja katika miongo miwili ya hivi karibuni.

Kwa muktadha huo uwepo wa Wakristo nchini Iraq ambao wanaishi katika mazingira ambayo sio mwafaka hususan kutokana na maeneo yao kuandamwa na vitendo vya utumiaji mabavu ni sababu kuu ya Papa Francis kufanya safari katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Mazungumzo ya Papa Francisi na Ayatullah Sayyid Ali Sistani (Jumamosi 06.03.2021)

 

Akiwa mjini Baghdad kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani aliwataka Wairaq kuithamni jamii ya wafuasi wa dini za walio wachache na kuamiliana na ndugu zao Wakristo kama “rasilimali yenye thamani”. Dakta Muhammad Masjid Jamaei, balozi wa zamani wa Iraq huko Vatican na Morocco na mtafiti wa masuala ya ulimwengu wa Kiarabu anasema kuwa, hatua hii ya Papa ya kufanya safari nchini Iraq itapelekea kuimarika nafasi ya Wakristo nchini Iraq na katika eneo kwa ujumla.

Sababu ya tatu ni kuwa, Iraq ni moja ya nchi muhimu zaidi za Kiislamu ulimwenguni ambayo wakazi wake wengi ni Mashia. Katika upande mwingine, Iraq ni mwenyeji wa mmoja wa Mamarjaa wakubwa wa Kishia ulimwenguni yaani Ayatullah Sayyid Ali Sistani ambaye anaungwa mkono na Mashia wote ulimwenguni. Papa Francis naye kwa upande wake ni mmoja wa viongozi wakubwa zaidi wa kidini ulimwenguni. Kwa muktadha huo, mazungumzo baina ya viongozi wawili wakubwa wa kidini ni moja ya sababu kuu za safari ya Papa Francis nchini Iraq.

Papa Francis, atembelea mahala alipozaliwa Nabii Ibrahim (as)

 

Sababu ya nne ya Kiongzoi wa Kanisa Katoliki Duniani kuichagua Iraq kwa ajili ya safari yake wakati huu ni hali ya sasa inayokabiliwa nayo nchi hiyo ambayo haidhirishi hasa upande wa kijamii. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, Iraq imeshuhudia machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vya aina mbalimbali vikiwemo vile vilivyo dhidi ya makundi ya kidini. Safari ya Papa Francis nchini Iraq ni sisitizo la ulazima wa kuweko mazungumzo kwa minajili ya kuhitimisha vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya makundi ya kidini, suala ambalo limetiliwa mkazo katika mazungumzo yake na Ayatullah Sistani.

Kwa kuzingatia mazingira haya tunaweza kusema kuwa, safari ya Papa nchini Iraq ina malengo maalum ambayo yanaonyesha nafasi ya kidini na bila kusahau mazingira yasiyo mazuri ya kijamii ya nchi hiyo hivi sasa; na hakuna malengo maalum ya kisiasa yanayofuatiliwa katika safari hiyo na katika mazungumzo baina ya viongozi wawili wa Kikristo na Kiislamu.