Badr: Marekani inakula njama ya kuwarejesha magaidi Iraq
Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Badr katika mkoa wa al-Anbar nchini Iraq amesema Marekani inapanga njama ya kuwarejesha magaidi katika mikoa ya magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Qusai al-Anbari amenukuliwa akisema hayo usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa, mpango huo wa Marekani wa kutaka kuwarejesha magaidi katika mikoa ya al-Anbar, Diyala, Nainawa na Salah al-Din unakusudia kuzidhoofisha harakati za kujitolewa wananchi wa Iraq (Hashdu Shaabi).
Ameeleza bayana kuwa, wapiganaji wa harakati hizo za muqawama kamwe hawataruhusu ndoto hizo za Marekani za kutaka kuwarejesha magaidi nchibni Iraq zitimie.
Kiongozi huyo wa Shirika la Badr ameongeza kuwa: Uhasama wa vikosi vya Marekani dhidi ya Hashdu Shaabi unatokana na kusimama kidete harakati hii ya muqawama, na kuzuia kurejeshwa nchini Iraq magenge ya kigaidi. Hii ndiyo sababu ya Marekani kushadidisha propaganda katika vyombo vya habari na mashambulio dhidi ya harakati hii.
Wiki iliyopita, Rais Barham Salih wa Iraq alitangaza kuwa, uamuzi umeshachukuliwa kuhusu kuhitimisha kuwepo kwa vikosi vya jeshi vamizi la Marekani nchini humo, na kwamba kwa hivi sasa idadi ya askari hao haizidi elfu mbili na mia tano.
Askari wa jeshi vamizi la Marekani wamepiga kambi nchini Iraq tangu mwaka 2003, wakati wananchi na makundi mbali mbali ya Iraq yameshapaza sauti mara kadhaa kutaka askari hao waondoke, huku bunge la Iraq likiwa limeshapitisha mpango tangu Januari mwaka 2020 kuhusiana na kuondoka askari hao katika ardhi ya nchi hiyo.