Uchaguzi wa Rais wa Syria kufanyika mwezi ujao wa Mei
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i69190-uchaguzi_wa_rais_wa_syria_kufanyika_mwezi_ujao_wa_mei
Syria imeanisha Mei 26 mwaka huu kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Rais katika taifa hilo la Kiarabu linalosakamwa na mapigano, hujuma za kigaidi na uingilaji wa kigeni kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 18, 2021 22:16 UTC
  • Uchaguzi wa Rais wa Syria kufanyika mwezi ujao wa Mei

Syria imeanisha Mei 26 mwaka huu kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Rais katika taifa hilo la Kiarabu linalosakamwa na mapigano, hujuma za kigaidi na uingilaji wa kigeni kwa zaidi ya muongo mmoja sasa.

Hayo yalitangazwa jana Jumapili na Spika wa Bunge la Syria, Hamouda Sabbagh na kuongeza kuwa, watu wenye azma ya kugombea kiti hicho wana fursa ya kuwasilisha maombi yao ndani ya muda wa siku kumi kuanzia leo Jumatatu.

Sabbagh ameongeza kuwa, miongoni mwa masharti kwa wagombea wa urais katika uchaguzi huo wa mwezi ujao, ni kwamba lazima wawe wameishi nchini Syria kwa muda wa miaka kumi mfululizo, mbali na kuwa na uungaji mkono wa angalau wabunge 35.

Wadadisi wa mambo wanasema kufanyika uchaguzi huo wa rais kutakuwa ni ushindi mwingine kwa taifa hilo na utakuwa ni sababu ya kupungua uingilaji wa kigeni kama ambavyo utaongeza kasi pia mchakato wa kuijenga upya nchi hiyo ya Kiarabu.

Rais Bashar al-Assad (55) aliibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 88 ya kura katika uchaguzi uliopita wa urais uliofanyika mwaka 2014.

Rais Bashar akishiriki zoezi la upigaji kura huko nyuma

Ikumbukwe kuwa, Julai mwaka jana 2020, uchaguzi wa Bunge la Syria linalojulikana kwa jina la "Majlis al Sha'ab" (Baraza la Wananchi) ulifanyika katika majimbo 15 ya uchaguzi, ambapo wananchi wa Syria walishiriki katika uchaguzi huo ili kuchagua wabunge 250 wa kuwawakilisha katika baraza hilo.

Licha ya kupita zaidi ya miaka 10 ya vita vya Syria, lakini njama za wapinzani wa serikali, magaidi na waungaji mkono wao wa nchi ajinabi si tu hazijaweza kuuondoa madarakani utawala halali wa nchi hiyo; bali sasa serikali ya Damascus inadhibiti zaidi ya asilimia 90 ya jiografia ya Syria.