Abbas aakhirisha uchaguzi wa bunge Palestina, ghasia zaibuka
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas ametangaza rasmi kuakhirisha uchaguzi wa bunge la Palestina uamuzi ambao umeibua hasira na ghasia.
Katika taarifa mapema leo Ijumaa, Abbas amesema uchaguzi huo umeakhirishwa kutokana na kuwa kwa sasa hauwezi kufanyika katika mji wa Quds (Jerusalem) Mashariki unaokaliwa kwa mabavu na Israel na ambao umeshuhudia ghasia siku za hivi karibuni.
Abbas amesema ataendelea kushauriana na makundi ya Palestina, ikiwemo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, HAMAS, kuhusu kadhia ya kufanyika uchaguzi Quds.
Uchaguzi huo ulikuwa unatarajiwa kuwa wa kwanza wa bunge la kitaifa Palestina katika kipindi cha miaka 15 na sasa haijulikani utafanyika lini.
"Kutokana na hali ngumu iliyopo, tumeamua kuakhirisha uchaguzi hadi tutakapopata hakikisha kuwa watu wa Quds watashiriki," amesema Abbas.
Uchaguzi wa bunge la Palestina ulikuwa umepangwa kufanyika Mei 22, 2021 baada ya hapo uchaguzi wa rais ulikuwa umepanga kufanyika Julai 31.
Makundi ya Palestina kama vile Hamas na Jihad Islami yamesusia kikao cha Ramallah cha kutangaza kuakhirishwa uchaguzi huo.
Msemaji wa Hamas Abdul Latif al Qanu amesema harakati hiyo inapinga kuakhirishwa uchaguzi kwani ni haki ya Wapalestina.
Maandamano yamefanyika katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Ghaza kupinga hatua ya Abbas kuakhirisha uchaguzi huo ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu.
Wakuu wa utawala haramu wa Israel hawakutaka kuona uchaguzi huo unafanyika na kwa msingi huo wamechochea na kuibua ghasia katika eneo la Quds.
Wazayuni na waitifaki wao katika nchi za Magharibi wanahofia kuwa huenda harakati ya Hamas ikapata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge Palestina huku harakati ya Fath ya Abbas ikitarajiwa kupata pigo katika uchaguzi huo.