May 13, 2016 07:49 UTC
  • Shambulizi la bomu la Daesh laua askari 17 nchini Iraq

Kwa akali askari 17 wa jeshi la Iraq wameuawa katika shambulizi la bomu lililofanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika mkoa wa Anbar, magharibi mwa nchi hiyo.

Duru za kijeshi zinaarifu kuwa, magaidi hao jana Alkhamisi walilishambulia kwa mabomu gari la kijeshi katika wilaya ya Jarayshi, yapata kilomita 10 kutoka Ramadi, makao makuu ya mkoa wa Anbar na kuua askari 17 wa jeshi la serikali. Imearifiwa kuwa, lengo la hujuma hiyo ya matakfiri wa Daesh ni kukata mawasiliano kati ya eneo la Ramadi na Tharthar, lililoko kilomita 120 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Baghdad ili kuwazuia wanajeshi wa Iraq kusonga mbele na kukomboa maeneo ambayo yanadhibitiwa na kundi hilo la kigaidi.

Aidha raia wawili waliuawa jana Alkhamisi katika hujuma tofauti ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika eneo la al-Obeidi, mashariki mwa Baghdad.

Hujuma za jana zimefanyika siku moja baada ya magaidi hao kutekeleza shambulizi jingine lililosababisha makumi ya watu kupoteza maisha.

Siku ya Jumatano, watu wasiopungua 64 waliuawa na wengine zaidi ya 85 kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea karibu na soko la Urayda katika kitongoji cha Sadr mashariki mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad.

Tags