Ayatullah Sistani ataka mataifa huru duniani yaunge mkono taifa la Palestina
Marjaa mkuu wa Kishia nchini Iraq kwa mara nyingine tena ametangaza uungaji mkono wake kwa 'mapambano ya kishujaa ya taifa lenye heshima la Palestina' katika kukabiliana na Wazayuni maghasibu na kutoa wito kwa mataifa yote huru duniani kuwaunga mkono Wapalestina.
Taarifa ambayo imetolewa na Ofisi ya Ayatullah Sistani, imesema: "Utumiaji mabavu ambao umeshuhudiwa hivi karibuni katika Msikiti wa Al Aqsa na maeneo mengine ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu bila shaka unaoneysha muqawama wa Wapalestina mkabala wa ukatili na unyama wa wavamizi na pia uvamizi huo unaoendelea ni ishara kuwa maghasibu hawako tayari kuondoka katika ardhi walizopora."
Ayatullah Sistani pia katika mkutano wake na Papa Francis Kiongozi wa Kanisa Katoloki duniani aliyetembelea Iraq mwezi Machi alikumbusha kuhusu kadhia ya Palestina na kusema kadhia hiyo ni mfano wa wazi wa kudhulumiwa na kukandamizwa taifa.
Katika siku za karibuni utawala ghasibu wa Israel umezidisha hujuma na mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Quds inayokaliwa kwa mabavu.
Wapalestina wasiopungua 208 walijeruhiwa Ijumaa iliyopita iliyosadifiana na maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika hujuma na mashambulizi ya wanajeshi wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Quds na katika kitongoji cha Sheikh Jarrah.
Tangu ulipoanza mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huu, Wapalestina wa mji wa Baitul-Muqaddas wameshuhudia kuongezeka hujuma na mashambulio dhidi yao yanayofanywa na wanajeshi wa Israel na hivyo kukwamisha harakati zao za kidini na kiibada katika mwezi huu tukufu.