Israel yaendeleza hujuma Ghaza, Wapalestina 109 wameuawa shahidi
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendeleza hujuma ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza Alhamisi usiku ikiwa ni muendelezo wa jinai zake dhidi ya Wapalestina wanaoishi katika eneo hilo. Wapalestina zaidi ya 109 wanaripotiowa kuuawa shahidi katika uvamizi wa Israel dhidi ya Ghaza katika kipindi cha siku chache zilizopita. Taarifa zinasema askari wa Kizayuni sasa wanatekeleza uvamizi wa nchi kavu dhidi ya Ghaza
Kwa mujibu wa taarifa, ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel zimedondosha mabomu katika eneo la makazi ya raia huko Al Barij kati mwa Ghaza usiku wa kuamkia leo ambapo Wapalestina wengine watatu wameuwa shahidi.
Halikadhalika jeshi la nchi kavu la utawala dhalimu wa Israel limeingia Ukanda wa Ghaza mapema leo asubuhi huku Harakati ya Mapambano ya Kiislamu Palestina, Hamas, ikutahadharisha kuwa itakakbiliana vikali na wanajeshi hao vamizi wa Israel.
Wizara ya vita ya Israel imetangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa majeshi yake ya angani na nchi kavu yanatekeleza hujuma dhidi ya Ghaza.
Waziri wa vita wa utawala huo vamizi Benny Gantz ametuma askari 9,000 katika mpaka wa Ghaza na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ambazo zimepachikwa jina la Israel.
Hatahivyo, baadhi ya vyombo vya habari vya Kizayuni vimekanusha kuwa askari wa Israel wameingia Ghaza.
Wakati huo huo, hadi sasa Wapalestina 109, wakiwemo watoto 28, wameuawa shahidi tokea Jumatatu wakati utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha mashambulizi dhidi ya Ghaza huku wengine 580 wakiwa wamejeruhiwa.
Utawala ghasibu wa Israel ulianzisha uvamizi dhidi ya Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hii kuandamana kulalamikia vikali ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina katika mji wa Quds (Jerusalem). Kitendo cha askari katili wa Israel kuuvamia Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds na kuwahujumu Wapalestina waliokuwa wakiswali katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kimehesabiwa kuwa ni kuvuka mstari mwekundu wa Wapalestina na Waislamu duniani.
Katika kujibu jinai hizo za Israel makundi ya kupigania ukombozi wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza yamevurumisha mamia ya makombora katika miji ya Israel ukiwemo mji wa Tel Aviv na kusababisha hasara kubwa. Waisraeli wasiopungua 7 wameangamizwa katika oparesheni hizo za ulipizaji kisassi za Wapalestina.