Utendaji wa mataifa ya Kiarabu kuhusiana na vita vya Quds
Vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza vilianza Jumatatu iliyopita.
Jumuiya ya Ulinzi wa Kiraia huko Gaza ilitangaza Jumamosi ya jana kwamba, kufuatia vita hivyo, hadi sasa Wapalestina 139 wameuawa shahidi ambapo 39 kati yao ni watoto na 22 ni wanawake. Wizara ya Afya ya Palestina nayo ilitangaza Ijumaa iliyopita kwamba, kwa akali watu 950 wamejeruhiwa katika mashambulio ya utawala haramu wa dhidi ya Ukanda wa Gaza. Katika mazingira haya kunaibuka swali hili kwamba, mataifa ya Kiarabu yamekuwa na radiamali gani kwa vita vya Israel dhidi ya Gaza? Ili kujibu swali hili tunapaswa kuyagawa mataifa ya Kiarabu katika makundi matatu.
Kundi la kwanza ni la mataifa ya Kiarabu ambayo yamejitokeza na kulaani vita hivyo. Nchi hizi ni nyingi na miongoni mwazo ni utawala wa Saudi Arabia ambao umetoa taarifa na kulaani vita hivyo. Kimsingi ni kuwa, kundi la kwanza la nchi hizi hazijachukua hatua yoyote ya maana ghairi ya kutosheka tu na kulaani kwa mdomo na kutochukua hatua ya kuwasaidia Wapalestina. Msimamo huo unaonekana hata kwa nchi kama Jordan ambayo imekuwa ikidai zaidi kuwaunga mkono wananchi wa Palestina ikilinganishwa na mataifa mengine ya Kiarabu.
Nchi hii nayo haijachukua hatua ya kivitendo ya kuwasaidia Wapalestina. Hali hii imeendelea kushuhudiwa licha ya kupita siku sita tangu kuanza vita hivyo na huku zaidi ya Wapalestina 1,100 wakiwa wameuawa shahidi na kujeruhiwa. Pamoja na hayo yote, lakini asasi za Kiarabu ikiwemo Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ambayo Palestina ni mwanachama wake, nayo hata haijaitisha kikao cha kujadili hali hii inayomkabili mmoja wa wanachama wake.
Kundi la pili ni mataifa ya Kiarabu ambayo yametoa radiamali na kufanya juhudi za kuhakikisha panatekelezwa usitishaji vita. Kundi hili linajumuisha nchi kama Misri na Qatar. Juhudi za kuweko usitishaji vita licha ya kuwa ni hatua ya kidiplomasia, lakini hazimalizi kiini cha tatizo na chanzo cha vita na mapigano. Nii jambo lisilo na shaka kuwa, usitishaji vita utapata maana halisi ya neno lenyewe pale utawala vamizi wa Israel utakapokomesha vitendo vyake vya utumiaji mabavu na jinai zake dhidi ya Wapalestina wa Quds. Katika juhudi zinazofanyika za kuweko usitishaji vita, hakuonekani ishara zozote za Israel kurejea nyuma na kukomesha unyama na mauaji yake dhidi ya Wapalestina huko Quds.
Saadullah Zarii, mweledi wa masuala ya Asia Magharibi anasema kuwa: Utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwa na lengo la kusimamisha vita umekimbilia kuiomba msaada Misri, Qatar na mhimili wa Magharibi. Hata hivyo hilo halijakuwa na natija; kwani licha ya Misri kuung'ang'ania muqawama wa Palestina usitishe vita, lakini wanamapambano hao wamekataa katakata ombi hilo. Wanamapambano wa Palestina wametangaza kuwa, licha ya kuwa kufikia tamati mashambulio ya Wazayuni huko Gaza ni mafanikio, lakini mara hii Israel inapaswa kuacha milele na daima hujuma zake dhidi ya wakazi wa Quds.
Kundi la tatu, ni nchi za Kiarabu ambazo hazijalaani hujuma za Israel dhidi ya Wapalestina na wala hazijachukua hatua yoyote ya kusitishwa vita hivyo. Kundi hili linajumuisha nchi za Imarati na Bahrain. Kimsingi ni kuwa, mataifa ya Kiarabu ambayo katika kipindi cha takribani mwaka mmoja uliopita yalitekeleza mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, hivi sasa yamenyamazia kimya jinai hizo, hatua ambayo kwa namna fulani inahesabiwa kuwa ni kuiunga mkono Israel.
Hapana shaka kuwa, jinai za sasa za utawala haramu wa Israel na kuuliwa shahidii na kujeruhiwa takribani Wapalestina 1,100, ni matokeo ya mpango mchafu wa Muamala wa Karne na hatua ya madola yaliyowasaliti Wapalestina pale yalipoamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.
Nukta ya mwisho ni hii kwamba, kuwa na msimamo legevu baadhi ya mataifa ya Kiarabu, kufanya juhudi za kufikiwa usitishaji vita pasi na kurejea nyuma Israel na vilevile kunyamaza kwa lazima au kwa ajili ya kutoa uungaji mkono kunakofanywa na baadhi ya mataifa ya Kiarabu ni sababu ya Israel kushadidisha jinai zake dhidi ya Wapalestina.
Baadhi ya mataifa hayo yamekwenda mbali zaidi na kukabidhi vyombo vyao vya habari kwa utawala dhalimu wa Israel ili uvitumie kueneza propaganda na kuyapaka matope makundi ya muqawama ya Palestina yanayopigana kutetea radhi na taifa lao.
Taqir Salami, msemaji wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina huko Gaza anasema: Baadhi ya vyombo vya habari vya Kiarabu vimekuwa vikiwaalika na kuwa wenyeji wa wahalifu wauaji na maafisa wa jeshi vamizi la Israel; na Wazayuni hao hutumia fursa ya vipindi hivyo kwa ajili ya kujisafisha na tuhuma za ugaidi na mauaji dhidi ya watu wasio na hatia na watoto wa Palestina. Ameongeza kuwa, moja ya madai machafu na uongo ambao unaenezwa na wauaji hao ni kwamba, eti wanamapambano wa Palestina wamekuwa wakiwatumia raia kama ngao yao. Wanasema uongo huo ili kuhalalisha mauaji yao yaliyoratibiwa dhidi ya wanachi wasio na hatia wa Palestina wakiwemo wanawake, watoto na wazee na kuvipeleka vita upande wa miji na makazi ya watu.