Wananchi wa Syria wafurahia ushindi wa Bashar al Assad, Wamagharibi wahamaki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i70630-wananchi_wa_syria_wafurahia_ushindi_wa_bashar_al_assad_wamagharibi_wahamaki
Baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini Syria ambapo Rais Bashar al Assad kwa mara nyingine ameshinda katika uchaguzi huo, wananchi wa maeneo mbalimbali ya Syria wamemiminika mitaani kusherehekea ushindi.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
May 28, 2021 02:25 UTC
  • Wananchi wa Syria wafurahia ushindi wa Bashar al Assad, Wamagharibi wahamaki

Baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini Syria ambapo Rais Bashar al Assad kwa mara nyingine ameshinda katika uchaguzi huo, wananchi wa maeneo mbalimbali ya Syria wamemiminika mitaani kusherehekea ushindi.

Wananchi wa Syria wamekesha katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kufurahia ushindi mutlaki wa Rais Bashar al Assad baada ya Spika wa Bunge la nchi hiyo kutangaza kuwa, Rais Bashar al Assad ameshinda uchaguzi huo kwa asilimia 95.1 ya kura za ndani na nje ya Syria.

Hata hivyo baada ya uchaguzi mkuu wa Syria kufanyika kwa ufanisi wa hali ya juu na kujitokeza idadi kubwa ya wananchi katika uchaguzi huo, nchi za Magharibi zimezidi kuonesha udumilakuwili wao kwa kuwawekea vikwazo wananchi hao kwa sababu ya kutumia haki yao ya kidemokrasia. Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Baraza la Ulaya limeongeza muda wa vikwazo dhidi ya wananchi wa Syria kwa mwaka mmoja zaidi.

Mwananchi wa Syria akitumbukiza kura yake kwenye sanduku la kura

 

Katika taarifa yake, Baraza la Ulaya limesema kuwa, vikwazo walivyowekewa wananchi wa Syria tangu mwaka 2011 vimerefushwa kwa muda wa mwaka mmoja zaidi. Vikwazo hivyo vinahusu mashirika ya biashara, mashirika ya mafuta, sekta ya uwezekezaji pamoja na kuzuia mali za Benki Kuu ya Syria zilizoko barani Ulaya.

Uchaguzi Mkuu ulifanyika juzi Jumatano katika kona zote za Syria na idadi kubwa sana ya wananchi walijitokeza kwenye uchaguzi huo ili kutoa pigo jingine kwa maadui wasiolipendea kheri taifa hilo la Kiarabu. 

Vyombo vya habari vimerusha hewani picha za wimbi kubwa la wananchi wakishiriki katika upigaji kura kwa uhuru kamili nchini Syria suala ambalo ni ushindi mkubwa kwa mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Nchi za Ulaya ziemshindwa kuzuia hamaki zao kutokana na pigo hilo lililotolewa na wananchi wa Syria kwa madola ya kibeberu. 

Hata hivyo, vitendo hivyo vya kindumilikuwili vya nchi za Ulaya vimejibiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal al Miqdad ambaye amesema kuwa, nchi za Magharibi hazipaswi kujipa uthubutu wa kuzungumzia uchaguzi wa nchi hiyo kwani hauzihusu kwa mbali wala kwa karibu nchi hizo za kibeberu.