Saudia yapanga kuwanyonga vijana 40 wa Kishia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i71442-saudia_yapanga_kuwanyonga_vijana_40_wa_kishia
Wanaharakati wa haki za binadamu wameonya kuwa, utawala wa Aal-Saud unapanga kuwanyonga makumi ya vijana Waislamu wa madhehebu ya Shia mkoani Qatif mashariki mwa Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 19, 2021 08:07 UTC
  • Saudia yapanga kuwanyonga vijana 40 wa Kishia

Wanaharakati wa haki za binadamu wameonya kuwa, utawala wa Aal-Saud unapanga kuwanyonga makumi ya vijana Waislamu wa madhehebu ya Shia mkoani Qatif mashariki mwa Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Saudi Leaks, zaidi ya vijana 40 wanakodolewa macho na hukumu ya kuuawa kwa kunyonga, kwa kushiriki tu maandamano mwaka 2011 katika mkoa Qatif ambao aghalabu ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, mashariki mwa Saudi Arabia.

Jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu hivi karibuni zililaani vikali kitendo cha Riyadh kutekeleza hukumu ya kifo dhidi ya kijana Mustafa Mustafa al-​Darwish (26).

 

Chinjachinja ya Saudia

Maafisa wa Saudia walimbambikizia kijana huyo tuhuma 13, ya chini kabisa ikiwa ni kushiriki katika maandamano ya watu wa Qatif mwaka 2021 dhidi ya utawala wa kifalme. Watawala wa Riyadh walimkamata kijana huyo Mei 2015 akiwa na umri wa miaka 17 pekee.

Saudi Arabia ni miongoni mwa nchi zinazoongoza dunia kwa kunyonga watu na imekuwa ikilaumiwa sana kutokana na rekodi yake mbaya ya kukanyaga haki za binadamu na kuua wanaharakati na wapinzani wa sera na siasa za utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal-Saud.   Maelfu ya wanaharakati, mashekhe na watetezi wa haki za kiraia wanashikiliwa katika korokoro za Saudi Arabia.