Mamluki wa Saudia wauawa katika mashambulio ya makombora ya Yemen
Makumi ya mamluki wa muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia wameuawa na kujeruhiwa katika mashambulio ya makombora ya jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya Wayemen katika mkoa wa Ma'arib, katikati mwa hiyo maskini ya Kiarabu.
Msemaji wa vikosi vya jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema hayo leo Jumatano katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, makumi ya mamluki wa muungano vamizi nchini humo unaoongozwa na Saudia wameuawa na kujeruhiwa baada ya makundi ya kujitolea ya wananchi kuvurumisha makombora dhidi ya kambi za wavamizi katika mkoa huo wa kistratajia.
Ameongeza kuwa, mamluki kadhaa wa muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia wameangamizwa baada ya vikosi vya Yemen kutekeleza shambulio la kombora la Badr-1 lililolenga mkusanyiko wa makanda wa muungano huo katika kambi ya jeshi ya Sahn al-Jin.
Jenerali Saree amebainisha kuwa, mamluki wengine kadhaa wameuawa na kujeruhiwa katika shambulio la pili lililolenga kambi ya Kikosi cha Tatu cha muungano huo wa kijeshi nje kidogo ya mkoa wa Ma'arib.
Amefafanua kuwa, vikosi vya Yemen vimetekeleza mashambulio hayo kulipiza kisasi, baada ya muungano huo wa Saudia kufanya hujuma za anga zilizolenga wilaya za Majzar na Sirwah katika mkoa huo jioni ya jana Jumanne.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, jeshi la Yemen lilitangaza habari ya kuangamiza na kujeruhi makumi ya wanajeshi wa utawala huo wa kifalme huko kusini mwa Saudi Arabia. Katika operesheni hiyo, wanajeshi wa Yemen walifanikiwa kudhibiti kikamilifu maeneo ya miinuko ya MBC, al Fukhaidha, al-Qambora, al-Amoud, Tawaleq na al Baydah, na mashariki mwa Qa’im Sayab, katika eneo hilo la Jizan.