Israel yaiomba Marekani iakhirishe kufungua ubalozi wake Quds
Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameiomba Marekani iakhirishe kufungua tena ubalozi wake mdogo huko Baytul Muqaddas hadi baadaye ili isiutie utawala huo katika mazingira magumu ya kisiasa.
Maafisa hao wa utawala wa Kizayuni wamesema kuwa, Israel imeiomba Marekani kutoendelea mbele na mpango wake wa kufungua tena ubalozi wake mdogo huko Quds hadi mwishoni mwa msimu wa mwaka huu wa joto ili kuipunguzia mashinikizo ya kisiasa serikali ya Tel Aviv.
Mtandao wa habari wa Walla wa utawala wa Kizayuni umeongeza kuwa, Wamarekani wanaelewa hali halisi ilivyo hivi sasa na kwamba inawezekana suala la kufungua tena ubalozi wao mdogo huko Quds likaakhirishwa hadi mwezi Septemba.
Mwezi Mei mwaka huu, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken alisema kuwa, Washington ina nia ya kufungua tena ubalozi wake mdogo huko Quds baada ya ubalozi huo kufungwa na utawala wa Donald Trump mwaka 2019.
Mwezi Mei mwaka huu, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni, alimuomba Blinken asifungue tena ubalozi mdogo wa Marekani huko Quds, na badala yake afungue Ramallah au katika mji wa Abu Dis. Hata hivyo waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani alikataa na kusema kuwa, serikali ya hivi sasa nchi hiyo ina nia ya kufungua tena ubalozi wake mdogo katika mji wa Quds.
Mtandao huo wa habari wa Walla wa utawala wa Kizayuni umedai pia kuwa, wakati huo Netanyahu alimwambia Blinken kuwa amepanga kulitumia kisiasa suala hilo lakini Marekani ilikataa. Ikumbukwe kuwa Marekani ndiye muungaji mkono mkuu wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, ingawa baadhi ya wakati utekelezaji wa viongozi wa Marekani hubadilika kwa sababu za kisiasa.