Joe Biden: Wanajeshi wote wa Marekani kuondoka Afghanistan ifikapo Agosti 31
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i72190-joe_biden_wanajeshi_wote_wa_marekani_kuondoka_afghanistan_ifikapo_agosti_31
Serikali ya Marekani imetangaza kuwa, zoezi la kuwaondoa wanajeshi wake walioko nchini Afghanistan linatarajiwa kumaliza ifikapo tarehe 31 ya mwezi ujao wa Agosti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 10, 2021 03:01 UTC
  • Joe Biden: Wanajeshi wote wa Marekani kuondoka Afghanistan ifikapo Agosti 31

Serikali ya Marekani imetangaza kuwa, zoezi la kuwaondoa wanajeshi wake walioko nchini Afghanistan linatarajiwa kumaliza ifikapo tarehe 31 ya mwezi ujao wa Agosti.

Hayo yameelezwa na Rais Joe Biden ambaye amedai kwamba,  eti nchi yake ilipeleka majeshi huko  Afghanistan kwa ajili ya kukabiliana na wale waliohusika na mashambulizi ya Septemba 11 na Osama Bin Laden.

Marekani baada ya kukiuka mara kadhaa ahadi yake ya kuwaondoa wanajeshi wake huko nchini Afghanistan, sasa imetangaza kuwa, hadi kufikia Agosti 31 mwaka huu itakuwa imewaondoa wanajeshi hao kutoka nchini humo.

Marekani inaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan katika hali ambayo, kuwepo kwa wanajeshi hao kwa miaka 20 katika nchi hiyo hakujawa na natija yoyote ghairi ya mauaji ya makumi ya maelfu ya wananchi wa Afghanistan, kuhairibiwa miundomsingi ya nchi na kuongezeka pakubwa vitendo vya ugaidi na ukosefu wa usalama na amani.

Rais Joe Biden wa Marekani

 

Ikumbukwe kuwa, mnamo mwaka 2001, Marekani na waitifaki wake waliishambulia na kuivamia kijeshi nchi ya Afghanistan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kurejesha amani nchini humo; hata hivyo uvamizi huo uliitumbukiza Afghanistan kwenye lindi la vita na mapigano, kuangamiza miundomsingi yake ya kiuchumi  na kushamirisha machafuko, ugaidi na uzalishaji wa madawa ya kulevya katika nchi hiyo.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan kimsingi ni kukiri wazi kugonga mwamba mpango wa Washington katika nchi hiyo.