Kundi la Taliban lateka maeneo zaidi Afghanistan
Kundi la Taliban nchini Afghanistan limendelea kupambana na jeshi la serikali katika mikoa mitatu ya kaskazini mwa nchi hiyo ya Kunduz, Sar-e-Pul na Jawzjan huku taarifa zikisema raia wameuawa katika mapigano hayo.
Kundi la Taliban limedai leo kwamba limeuteka mji muhimu wa Afghanistan wa Kunduz. Mashirika kadhaa ya habari yamethibitisha kuwa mji wa Kunduz unashikiliwa na wapiganaji wa Taliban na kwamba wamechukua mitambo yote muhimu ya mji huo.
Shirika la Habari la TOLOO linasema majengo kadhaa ya mji huo sasa yanashikiliwa na Taliban na kwamba vikosi vya serikali viko mbioni kuwatimua wapiganaji wa kundi hilo.
Mbunge kutoka Sar-e-Pul ameliambia shirika la AFP kwamba kundi la Taliban limeingia mjini Kunduz na kwamba mapigano yanaendelea barabarani. Mji wa Kunduz umewahi kutekwa mara mbili na waasi wa kundi la Taliban, lakini kwa muda mfupi tu, na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2016.

Hayo yanajiri wakati ambao, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa wito kwa pande zote katika vita nchini Afganistan kusitisha vita na mauaji ya ndugu kwa ndugu sambamba na kufanya mazungumzo ya kutatua mgogoro uliopo huku ikitangaza kuwa tayari kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema Iran, sawa na miaka ya nyuma, inasimama pamoja na watu wa Afghanistan na iko tayari kuunga mkono suluhisho lololote lile ambalo litapelekea kumalizika vita vya zaidi ya miongo minne Afghanistan.