Haniya: Tunawashikilia mateka wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel
-
Ismail Haniya
Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema maudhui ya mateka wa vita bado iko mezani na kwamba Hamas inawashikilia mateka wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Ismail Haniya amesema katika mahojiano maalumu na televisheni ya al Alaam kwamba, Hamas iko katika hali ya vita kamili na Israel na kwamba kabla ya vita vya karibuni vya "Panga la Quds" kulitokea vita vingi vilivyoibua kadhia ya mateka wa vita kama Gilad Shalit ambaye alikuwa mateka wa Hamas kwa kipindi cha miaka 5, na aliachiwa huru mkabala wa kuachiwa huru mateka elfu moja wa Kipalestina na Kiarabu.
Haniya ameongeza kuwa, baada ya vita vya Panga la Quds Israel imefanya jitihada kubwa za kulifungamanisha suala la ujenzi mpya wa Gaza na kadhia ya kuachiwa huru mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa na Hamas na kutaka kusema kuwa, ukarabati wa eneo hilo lililoharibiwa na vita hautafanyika ila baada ya kuachiwa huru wanajeshi wa utawala huo wanaoshikiliwa mateka.
Mkuu wa Idara ya Siasa ya Hamas amesema harakati hiyo imejibu kwa kusema kuwa suala la ukarabati wa Gaza halipaswi kufungamanishwa na kadhia ya mateka wa Kizayuni na kwamba ujenzi mpya wa Gaza unapaswa kufanyika bila ya masharti yoyote; kwa msingi huo Hamas haikubali kuporwa matunda ya "Panga la Quds" kwa panga la kuijenga upya Gaza.
Haniya amesema wanampambano wa Palestina hawatalegeza kamba na kuiacha mkono Quds mbele ya njama inayotumia kisingizio cha ujenzi mpya wa Gaza na kwamba kuulinda Msikiti wa al Aqsa na Quds ndio mhimili wa vita vijavyo na utawala haramu wa Israel.
Katika vita vya siku 12 vya Panga la Quds, utawala wa Kizayuni wa Israel uliwaua shahidi Wapalestina 255 wakiwemo watoto 66, wanawake 39 na wazee 17. Wapalestina wengine karibu elfu mbili pia walijeruhiwa.