May 19, 2016 03:57 UTC
  • Iran yalaani wimbi la mashambulizi ya kigaidi ya Daesh Iraq

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani wimbi la mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambalo limesababisha vifo vya mamia ya watu tokeo Jumatano ya wiki iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana Jumatano imelaani mashambulizi hayo ya kikatili na kuitaka jamii ya kimataifa kuisaidia nchi hiyo ya Kiarabu kukabiliana na zimwi la ugaidi. Kadhalika taarifa hiyo iliyotolewa na Hussein Jaber Ansari, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesema hatua ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ya kuua kinyama raia wa nchi hiyo, inaashiria namna matakfiri hao walivyoshindwa kupambana na jeshi la Iraq na vikosi vya kiraia vilivyojitolelea kukabiliana nao na kwa msingi huo, wamehiari kuwageukia wananchi wasio na hatia. Aidha amesema wimbi hilo la mashambulizi ya kigaidi lililoutukisa mji mkuu Baghdad na viunga vyake yanaonyesha namna kundi hilo linavyoendelea kupoteza udhibiti wa maeneo mengi yaliyokuwa chini yao. Zaidi ya watu 200 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika wimbi jipya la mashambulizi ya kigaidi lililotekelezwa na kundi la wakufurishaji wa Daesh katika maeneo mbali mbali ya Baghdad na viunga vyake, tokea Jumatano ya wiki jana. Aghalabu ya mashambulizi hayo ya kigaidi yamekuwa yakilenga maeneo ambayo akthari ya wakazi wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia, kama vile eneo la Sadr. Takwimu za serikali ya Baghdad zinaonyesha kuwa, kwa sasa magaidi wa Daesh wanadhibiti asilimia 14 ya ardhi ya Iraq, kinyume na asilimia 40 mwaka 2014.

Tags