Washington Post: Kusambaratika haraka Afghanistan ni sehemu ya kufeli kwa Marekani
Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa, kusambaratika haraka serikali ya Afghanistan mbele ya hujuma na mashambulizi ya kundi la Taliban ni sehemu ya kushindwa na kufeli kwa muda mrefu lakini kwa kimyakimya kwa Marekani.
Ripoti iliyochapishwa na gazeti hilo la Marekani imeashiria kusonga mbele haraka wapiganaji wa kundi la Taliban na kutekwa miji mbalimbali ya Afghanistan na kueleza kuwa, serikali zilizofuatana za Marekani ikiwemo serikali za George Bush, Barack Obama na Donald Trump zilikuwa zikificha ukweli kwamba, Marekani imeshindwa vita huko Afghanistan, na vinara wa White House na jeshi walikuwa wakifanya jitihada za kuzika na kuficha kabisa makosa yao.
Ripoti ya Washington Post imeongeza kuwa, kwa mujibu wa tathmini ya vyombo vya ujasusi vya Marekani, kusambaratika haraka vikosi vya jeshi la Afghanistan ambako kuna maana ya kundi la Taliban kudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul, yumkini kukatimia katika kipindi cha miezi mitatu na huenda hata katika kipindi cha wiki kadhaa zijazo. Ushindi wa Taliban unaandamana na kuondoka kundi la mwisho la wanajeshi wa Marekani na shirika la NATO huko Afghanistan.
Ripoti zinasema wapiganaji wa kundi la Taliban wanaendelea kuteka mikoa na maeneo mengi ya Afghanistan na mpaka sasa wameteka miji mikuu ya mikoa 18 ya nchi hiyo.