Ripoti: Ubalozi wa Marekani mjini Kabul waamuru wafanyakazi waharibu nyaraka nyeti
Ubalozi wa Marekani katika mji mkuu wa Afghanistan umewaamuru wafanyakazi wake waharibu nyaraka na kompyuta nyeti pamoja na nyenzo zingine ambazo zinaweza kutumiwa dhidi ya Marekani, kulingana na vyombo vya habari vya vya nchi hiyo ya Magharibi.
Maagizo hayo yametolewa katika barua iliyoandikwa kwa wafanyikazi katika ubalozi wa Marekani mjini Kabul.
Kwa mujibu wa taarifa ya Televisheni ya CNN, barua hiyo imewataka wanadiplomasia kuharibu kompyuta na nyaraka zingine nyeti kabla ya kuondoka, pamoja na vitu vyenye bendera ya nchi hiyo, nembo za ubalozi, na nakala zingine ambazo zinaweza kutumiwa vibaya katika juhudi za propaganda.
Barua hiyo inafichuliwa wakati kukiwa na taarifa kuwa kundi la Taliban linajiandaa kushambulia Kabul, mji mkuu. Aidha barua hiyo inakuja siku moja baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, kutangaza kuwa imepelekea wanajeshi 3,000 Afghanistan kwa ajili ya kuwahamisha wafanyakazi wa ubalozi wa nchi hiyo mjini Kabul, ikiacha wanadiplomasia wachache sana katika nchi hiyo. Kulingana na ripoti, uwezekano wa mji mkuu Kabul kutekwa katika wiki zijazo umetokana na mafanikio ya Taliban katika medani ya vita katika siku chache zilizopita.
Marekani ilivamia Afghanistan mnamo Oktoba 2001 na kuwaondoa Taliban madarakani. Vikosi vya Marekani vimeikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa takriban miaka 20 kwa kisingizio cha kuangamiza kundi la Taliban. Lakini baada ya wanajeshi wa Marekani na waitifaki wake kuondoka Afghanistan hivi karibuni, kundi la Taliban limeibuka tena kwa nguvu zake zote na sasa linapanga kuteka na kuudhibiti mji mkuu, Kabul.