UNICEF: Watoto milioni 11.3 wa Yemen wanahitajia misaada ya kibinadamu
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watoto milioni 11.3 wa Yemen wanahitajia misaada ya kibinadamu.
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) imeeleza kuwa, katika kipindi chote cha vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, nchi hiyo imekuwa ikikabiliwa na hali mbaya kabisa ya kibinadamu kiasi kwamba, watu milioni 20.7 ambao ni sawa na asilimia 71 ya wananchi wote wa nchi hiyo wanahitajia misaada ya kibinadamu.
Aidha hivi karibuni Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulionya kuwa, mustakabli wa elimu ya watoto zaidi ya milioni 6 nchini Yemen upo hatarini kwani watoto hao wamo katika hatari ya kukosa masomo kutokana na kushindwa kwenda shuleni.
Hivi sasa kuna watoto zaidi ya milioni mbili wenye umri wa kwenda shule ambao wameshindwa kufanya hivyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya kukosa shule kutokana na shule nyingi kubomolewa na mashambulio ya anga ya Saudi Arabia.

Utawala dhalimu wa Saudia ulianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mnamo Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia mjini Riyadh.
Hata hivyo hadi sasa Saudia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao kutokana na kusimama kidete wananchi wa Yemen wakiongozwa na Harakati ya Ansarullah.