Moscow: Madai ya Marekani kwamba imefanikiwa huko Afghanistan ni ndoto tupu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73612-moscow_madai_ya_marekani_kwamba_imefanikiwa_huko_afghanistan_ni_ndoto_tupu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia amesema kuwa madai ya Marekani kwamba imefanikiwa kutimiza malengo yake nchini Afghanistan ni ndoto tupu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 17, 2021 04:56 UTC
  • Maria Zakharova
    Maria Zakharova

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Russia amesema kuwa madai ya Marekani kwamba imefanikiwa kutimiza malengo yake nchini Afghanistan ni ndoto tupu.

Akijibu madai yaliyotolewa na Marekani kwamba imetimiza malengo yake nchini Afghanistan, Maria Zakharova amesema: Moja kati ya malengo yaliyotangazwa na Marekani huko Afghanistan ni kuliangamiza kundi la Taliban. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ameongeza kuwa, maafisa wa serikali ya Marekani wametoa madai mengi wakisema kuwa wamefikia malengo yao huko Afghanistan lakini kwa sasa wanapaswa kuulizwa kuhusu ndoto hiyo kwamba, malengo hayo ya awali yaliainishwa na nani? 

Kuhusu matamshi yaliyotolewa na msemaji wa Pentagon, John Kirby kwamba hawezi kuthibitisha picha zinazowaonesha raia wa Aghanistan wakidondoshwa chini kutoka kwenye ndege ya wanajeshi wa Marekani, Maria Zakharova amesema kuwa, inakuwa vipi Marekani inapata taarifa zinazohusiana na sumu na kemikali ya Novichok na taarifa za kina kuhusu wadukuzi wa Kirussia lakini inashindwa kutoa jibu kuhusu yaliyojiri kwenye mbawa na matairi ya ndege yake huko Afghanistan?

Itakumbukwa kuwa mitandao ya kijamii na vyombo vya habari jana vilionesha filamu ya ndege ya kijeshi ya Marekani iliyokuwa imepaa kutoka uwanja wa ndege wa Kabul ikidondosha chini watu wasiopungua wawili.

Kabul, Afghanistan

Baada ya kuikalia ardhi ya Afghanistan kwa kipindi cha miaka 20 Marekani imeshindwa kuliangamiza kundi la Taliban ambalo sasa limeshika tena madaraka ya nchi hiyo. Vilevile katika kipindi hicho cha kuwepo wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan ugaidi umekuwa na kupanuka zaidi, biashara na uzalishaji wa dawa za kulevya umeimarika na maelfu ya Waafghani wameuawa kutokana na machafuko yanayoigubika nchi hiyo.