Nasrallah: Marekani bado ina ujinga na inakariri makosa yake katika eneo
Kiongozi wa harakati ya Lebanon Hezbullah anasema kushindwa kwa Marekani nchini Afghanistan kunaonyesha ujinga wa wakuu wa Washington na kukosekana mahesabu katika sera zao za kigeni.
Sayyed Hassan Nasrallah amenukuliwa na mtandao wa televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon akisema hayo Jumanne, katika mkesha wa siku ya tisa ya maombolezo ya Muharram.
Nasrallah amesema "mandhari ya Kabul inafanana kabisa na mandhari ya Saigon huko Vietnam," na kwamba "Marekani bado ina sera za kijinga katika eneo, na inarudia makosa yale yale." Kiongozi wa Hezbullah amesisitiza kwamba Rais wa Marekani Joe Biden aliondoa majeshi yake kutoka Afghanistan "kwa sababu hangeweza tena kumudu" matokeo ya kubakia katika nchi hiyo.
Kiongozi wa Hizbullah amesema, "Biden alisema kuwa alitumia zaidi ya dola trilioni moja na sasa Wamarekani wameondoka wakiwa wamedhalilika na wameshindwaa," na kuongeza kuwa, "Biden alitaka vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Afghanistan kupitia vita kati ya vikosi vya Taliban na serikali ya Afghanistan. "
Nasrallah amesema vikosi vya muungano wa kijeshi NATO vikiongozwa na Marekani nchini Afghanistan "vimeshindwa vibaya," na kwamba kujiondoa kwa fedheha kwa Marekani katika nchi hiyo kunaonyesha kuwa Washington "haitapigana kwa niaba ya washirika wake."
Uvamizi ulioongozwa na Marekani dhidi Afghanistan kwa kisingizio cha kile kinachoitwa vita dhidi ya ugaidi uliwaondoa Taliban madarakani miaka 20 iliyopita, lakini hujuma hiyo ya kijeshi ilivuruga zaidi usalama wa nchi hiyo.
Kundi la Taliban hivi karibuni lilichukua haraka udhibiti wa miji mikubwa ya Afghanistan baada ya Biden kuamuru kuondolewa mara moja vikosi vya Marekani nchini humo.
Wanamgambo wa Taliban walizingira mji mkuu Kabul siku ya Jumapili, na kumlazimisha rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani, kukimbia nchi. Ghani, ambaye sasa hajulikani alipo, aliondoka Afghanistan wakati Taliban iliingia Kabul bila kupingwa.
Matukio hayo yalisababisha machafuko, na maelfu ya raia wa Afghanistan na wanadiplomasia wameondoka nchini humo.