Sayyid Nasrullah afichua njama ya Wamarekani huko Lebanon na Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73660-sayyid_nasrullah_afichua_njama_ya_wamarekani_huko_lebanon_na_afghanistan
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah jioni ya Jumanne iliyopita na katika mfululizo wa hotuba zake za mwezi wa Muharram alizungumzia yanayojiri eneo la Magharib mwa Asia hususan Lebanon na Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 18, 2021 21:48 UTC
  • Sayyid Nasrullah afichua njama ya Wamarekani huko Lebanon na Afghanistan

Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah jioni ya Jumanne iliyopita na katika mfululizo wa hotuba zake za mwezi wa Muharram alizungumzia yanayojiri eneo la Magharib mwa Asia hususan Lebanon na Afghanistan.

Kuhusiana na hali ya Lebanon, Sayyid Nasrullah amekanusha tena madai yanayotolewa dhidi ya Hizbullah na kusema harakati hiyo inashirikiana na serikali na jeshi la taifa kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa mgogoro wa uchumi hususan tatizo la nishati nchini Lebanon. Bila ya kutaja jina la mtu au watu maalumu, Katibu Mkuu wa Hizbullah amefichua kwamba: "Baadhi ya maafisa wa serikali ya Lebanon wamehusika katika kuibua mgogoro wa nishati nchini na wanashiriki katika kuficha uhalifu unaofanywa na walanguzi wa nishati." Kuhusu tuhuma zinazotolewa na baadhi ya vyombo vya habari na watu wenye mfungamano na mrengo wenye mielekeo ya Kimagharibi wa 14 Machi dhidi ya Hizbullah na Syria kwamba zinafanya magendo ya nishati, Sayyid Nasrullah amesema: "Baadhi ya watu wanafumbia jicho ulanguzi wa nishati na kujikita kwenye madai ya magendo ya bidhaa hiyo ili kuipaka matope Syria na waitifaki wake." Kwa sababu hiyo kwa mara nyingine tena amesisitiza kuwa: "Mtu yeyote anayedhani kuwa Hizbullah inafanya magendo ya nishati kuelekea Syria yumo katika makosa."

Wanamuqawama wa Hizbullah 

Vilevile ameashiria malengo ya vita vya kiuchumi nchini Lebanon na kusema: "Lengo la vita vya kiuchumi nchini Lebanon ni kulidhalilisha taifa na harakati ya mapambano ya Lebanon (Hizbullah) ili kuliweka taifa chini ya mashinikizo na kutengeneza mazingira ya kusambaratika nchi hii." Kwa msingi huo lengo kuu la vita vya kiuchumi na mashinikizo yanayofanywa dhidi  Lebanon ikiwa ni pamoja na kukwamisha mchakato wa kuundwa serikali mpya nchini humo, ni kutaka kusambaratisha nchi kwa kuwadhalilisha wananchi na kuzusha ghasia na machafuko.

Kuhusu masuala ya kikanda na matukio ya sasa huko Afghanistan, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amefichua njama inayopikwa dhidi ya nchi hiyo na kusema: "Rais Joe Biden wa Marekani alitaka kuanzishwa vita vya ndani nchini Afghanistan kupitia njia ya kuchochea mapigano baina ya jeshi la serikali na wapiganaji wa kundi laTaliban." 

Rais Joe Biden wa Marekani  

Vilevile ameashiria kuondoka majeshi ya Marekani huko Afghanistan na kusema kuwa, Rais wa Marekani amelazimika kuondoa majeshi yake nchini humo kwa sababu Marekani haiwezi tena kustahamili gharama za kuwepo wanajeshi wake nchini humo. Amesema, Biden ameweka wazi kuwa Marekani imetumia zaidi ya dola trilioni moja huko Afghanistan lakini imeshindwa na kuondoka nchini humo kwa madhila.

Sayyid Nasrullah ameashiria pia baadhi ya tawala za kanda ya Asia Magharibi zinazotaka kufikia malengo yao kwa kutegemea madola ya kigeni hususan Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: "Matukio ya Afghanistan yana umuhimu mkubwa, na mataifa ya kanda hii yanapaswa kuelewa vyema taathira zake za kistratijia. Biden amesema kwamba si kazi ya Marekani kupigana vita kwa niaba ya watu wengine; ujumbe huu unaelekezwa kwa wale wanaoisubiri Marekani ipagane kwa ajili yao.”

Taliban wakip;iga doria Kabul, mji mkuu wa Afghanistan 

Sehemu hii ya hotuba ya Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ni ujumbe wa wazi kwa wale ambao badala ya kutegemea nguvu za ndani ya nchi na wananchi wao, wanategemea madola ajinabi katika suala la kulinda usalama wao kupitia mipango kama ule wa “kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni” na kupuuza matukufu ya Waislamu.

Sehemu nyingine ya hotuba ya Sayyid Nasrullah ilisisitiza kuwa Marekani si nchi ya kuaminika na kutegemewa na kwamba, uhakika huu umedhihirika sasa huko Afghanistan baada ya serikali ya nchi hiyo kuachwa mkono na muitifaki wake huyo, na kwamba nchi nyingine za kanda hii zinazoiamini na kuitegemea Marekani pia zitakumbwa na hatima kama hiyo.