Hatua hatari ya Imarati kukaribisha nchini upenyaji wa kiusalama wa Israel
Vyombo vya habari vya utawala haramu wa Israel vimeripoti kwamba Imarati imeamua kutumia ndege zisizo na rubani za utawala huo katika kusimamia na kulinda usalama wa taasisi na miundomsingi yake.
Mwaka mmoja umepita tangu Umoja wa Falme za Kiarabu au Imarati itiliane saini na utawala ghasibu wa Israel mkataba wa pande mbili kuwa na uhusiano wa kawaida. Katika kipindi hiki, licha ya Imarati kufungua ubalozi wake mjini Tel Aviv pia imeimarisha uhusiano na utawala huo ghasibu katika nyanja nyingine. Mbali na Imarati kudai kwamba imeboresha uhusiano huo kwa lengo la kuimarisha amani na ushirikiano wa kieneo lakini ushahidi na mambo ambayo tayari yamefikiwa kati ya pande mbili yanathibitisha wazi kwamba lengo la kwanza ambalo viongozi wa utawala wa Kizayuni wanalifuatilia katika uhusiano huo ni kuwa na ushawishi mkubwa wa kiusalama katika nchi za Kiislamu na Kiarabu na hasa huko Imarati.
Katika uwanja huo, vyombo vya habari vya Kizayuni vimelinukuu gazeti la masuala ya kiuchumi la Globes kwamba shirika la Kizayuni la Percepto tayari limeiuzia Imarati ndege zisizo na rubani au droni kwa ajili ya kusimamia usalama wa visima vyake vya mafuta, viwanda vya umeme na miundomsingi mingine. Ndege hizo zina uwezo wa kuchukua picha tofauti katika nyakati zote za usiku na mchana na pia kutambua kasoro za kimitambo na kiusalama zilizopo katika taasisi hizo.
Hivi karibuni pia gazeti la Kizayuni la Haaretz lilivinukuu vyombo vya usalama vya utawala wa Israel vikisema kuwa Imarati imekuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa bidhaa na zana za kiusalama za Israel.
Hatua hiyo ya Imarati inachukuliwa kuwa hatari kubwa kwa kuzingatia nuka kadhaa muhimu.
Nukta ya kwanza ni kuwa kunufaika na huduma za kiusalama kunachukuliwa kuwa hatua ya kiakili na busara pale pande mbili zinapokuwa na uhusiano wa kidiploamasia wa muda mrefu. Hii ni katika hali ambayo Abu Dhabi na Tel Aviv zimekuwa na uhusiano huo kwa muda wa mwaka mmoja tu. Kwa msingi huo kuwa na uhusiano wa kiusalama katika mazingira hayo kunaweza kuwa na gharama kubwa.
Nukta ya pili ni kuwa kimsingi uhusiano wa Israel na nchi za Kiarabu sio wa kirafiki. Uadui wa Mayahudi na Waarabu ni moja ya migogoro mikubwa duniani na una historia ndefu. Hata kama Imarati haijawahi kuwa na ugomvi wala vita na Israel lakini ni wazi kuwa pande mbili hizo hazijaanzisha uhusiano wao kwa msingi wa urafiki bali ni kutokana na umri mfupi wa Imarati na udhaifu wake wa kijeshi. Kwa msingi huo Israel inaitazama Imarati kupitia kioo cha uhusiano wa Kiarabu na Kiyahudi na kinyume na ilivyo Abu Dhabi, haiamini nchi hiyo hata kidogo. Moja ya dalili za Israel kutoiamini Imarati ni Tel Aviv kupinga kuuziwa Abu Dhabi ndege za kivita za Marekani aina ya F35, hata baada ya kutiwa saini mkataba rasmi wa kuboreshwa uhusiano wa pande mbili.
Nukta ya tatu ni kwamba Israel ni utawala ulio na utambulisho wa uchokozi, tishio la usalama na vita. Iwapo kutatokea mvutano wowote wa muda mfupi au muda mrefu kati ya Abu Dhabi na Tel Aviv ni wazi kuwa ushawishi wa kiusalama wa Israel nchini Imarati unaweza kubadilika ghafla na kuwa tishio kubwa la kiusalama kwa nchi hiyo. Suala hilo ndilo lilizipelekea Misri na Jordan ambazo zilitiliana saini mkataba wa amani na utawala wa Israel katika miaka ya 1979 na 1994 kwa utaratibu kutotaka kuwa na uhusiano wa kiusalama na utawala huo.
Nukta ya mwisho ni kwamba Imarati haitumii tu huduma za Israel katika kudhamini usalama wa taasisi na viwanda vyake vya mafuta na nishati bali imekuwa ikitumia programu za kijasusi za Israel na hasa za Pegasus katika masuala ya usalama wa nchi hiyo. Kwa maneno mengine ni kwamba Imarati inatumia programu za Pegasus kufanya ujasusi dhidi ya raia wake. Ni kutokana na ukweli huo ndipo ushirikiano wa kiusalama kati ya Imarati na Israel ukaibua wasi wasi mkubwa miongoni mwa raia hao.