Hamas yasema Israel imefanya kosa kubwa, itateketea kwenye moto wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73796-hamas_yasema_israel_imefanya_kosa_kubwa_itateketea_kwenye_moto_wa_gaza
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, imelaani vikali mashambulio yaliyofanywa karibuni na utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kutahadharisha kuwa utawala huo umefanya makosa makubwa ya kimahesabu ambayo yataupelekea kuteketea katika moto mkali uliouwasha wenyewe katika ukanda huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 22, 2021 03:34 UTC
  • Hamas yasema Israel imefanya kosa kubwa, itateketea kwenye moto wa Gaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, imelaani vikali mashambulio yaliyofanywa karibuni na utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza na kutahadharisha kuwa utawala huo umefanya makosa makubwa ya kimahesabu ambayo yataupelekea kuteketea katika moto mkali uliouwasha wenyewe katika ukanda huo.

Taarifa ya Hamas imesema kwamba ni wazi kuwa walowezi wa Kizayuni wamefanya kosa kubwa la kutotathmini vyema hali ya mambo katika Ukanda wa Gaza, hawakuzingatia ujumbe wa wakazi wala wa harakati ya mapambano katika ukanda huo na kuamua kuwashambulia kwa ndege za kijeshi huku wakijeruhi waandishi, watoto na watu wengine katika ukanda huo.

Fawzi Barhoum, Msemaji wa Hamas amesema katika ujumbe huo leo Jumapili kwamba utawala ghasibu wa Israel unajaribu kufunika kushindwa kwake katika medani ya vita dhidi ya Wapalestina kwa kuwalenga watu wasio na hatia wala ulinzi. Amesema Gaza kwa mara nyingine itatetea kwa nguvu zake zote Msikiti wa al-Aqsa na maeneo mengine matakatifu na kumtokomeza adui kupitia mapambano matakatifu.

Fawzi Barhoum

Jumamosi usiku, ndege za kivita za Israel zilishambulia kwa mabomu maeneo kadhaa ya Ukanda wa Gaza ambapo Wapalestina wapatao 41 wamejeruhiwa, wawili wao wakiwa na majeraha makali.

Israel imedai kuwa ilifanya mashambulio hayo kulenga ghala la silaha la Hamas katika kujibu eti shambuliuo lililofanywa dhidi ya askari wake mmoja.