Muungano wa Saudia umeiba 85% ya mapato ya mafuta, gesi Yemen
Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita dhidi ya nchi hiyo maskini, umepora asilimia 85 ya mapato ya mauzo ya mafuta na gesi ya taifa hilo.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Al-Masirah, Mahdi Al-Mashat alisema hayo jana Jumapili katika mazungumzo yake mjini Sana'a na Abdel-Aziz bin Habtour, Waziri Mkuu wa Yemen na kueleza kuwa, viongozi wa nchi za muungano vamizi wa kijeshi hususan Marekani na Saudia, wanataka kurefusha mgogoro wa Yemen ili waendelee kupora mapato ya rasilimali chache za nchi hiyo.
Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amebainisha kuwa, muungano huo wa kijeshi haufuatilii kitu kingine ghairi ya kuwaongezea masaibu na matatizo wananchi wa Yemen, kupitia mzingiro wa kila upande usio wa kibinadamu dhidi ya nchi hiyo.
Al-Mashat ameeleza bayana kuwa, Washington inataka kudhoofisha thamani ya sarafu ya Yemen kupitia vita vya kiuchumi vinavyowalenga Wayemen wote.
Mapema jana, Adnan Al-Jarmozi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mafuta la Yemen alisema taifa hilo linahitaji tani milioni 1.36 za mafuta ya petroli, na tani milioni 1.54 za dizeli mwaka huu; lakini kufikia sasa limepokea tani 27,893 za petroli na 57,982 za dizeli.
Mbali na hasara hizo za mapato ya rasilimali, lakini vita hivyo vya kidhulma vya Saudia na waitifaki wake huko Yemen tokea Machi 2015 hadi sasa vimesababisha kuuliwa maelfu ya Wayemeni, kujeruhiwa makumi ya maelfu na kuwa wakimbizi mamilioni ya wengine.