UNICEF: Watoto milioni 10 Afghanistan wanahitaji msaada ili waendelee kubaki hai
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73860-unicef_watoto_milioni_10_afghanistan_wanahitaji_msaada_ili_waendelee_kubaki_hai
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF amesema, karibu watoto milioni 10 nchini Afghanistan wanahitaji misaada ya kibinadamu ili waweze kubaki hai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2021 22:18 UTC
  • UNICEF: Watoto milioni 10 Afghanistan wanahitaji msaada ili waendelee kubaki hai

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF amesema, karibu watoto milioni 10 nchini Afghanistan wanahitaji misaada ya kibinadamu ili waweze kubaki hai.

Henrietta Fore ameeleza katika taarifa aliyotoa Jumatatu kuhusiana na hali ya Afghanistan kwamba, karibu watoto milioni kumi wa Kiafghani wanahitaji msaada ili waweze kubaki hai; na kwamba inakadiriwa katika mwaka huu kuna watoto milioni moja wanaoteseka kwa lishe duni ambao kama hawatopatiwa huduma wataaga dunia.

Bi Fore ameongeza kwamba, takwimu zingine zinaonyesha kuwa, watoto milioni nne na laki mbili, wakiwemo wasichana milioni mbili na laki mbili wanashindwa kwenda skuli.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF amebainisha kuwa, "ni ukweli mchungu kwamba, mbali na watoto wa Kiafghani kukabiliwa na matukio ya kisiasa yanayojiri hivi sasa na mabadiliko ya kiutawala yaliyotokea nchini Afghanistan, tunakadiria kuwa masaibu yatakayowakumba watoto hao na akina mama katika miezi ijayo yataongezeka zaidi kutokana na ukame na uhaba mkubwa wa maji pamoja na athari haribifu za kijamii na kiuchumi zinazosababishwa na janga la Covid-19 na msimu ujao wa baridi kali.

Henrietta Fore

Bi Henrietta Fore amesisitiza kuwa UNICEF inaitaka Taliban na pande zingine nchini Afghanistan zitoe hakikisho kuwa shirika hilo na washirika wake wataweza kuendelea kutoa huduma za kibinadamu na kuwafikia watoto wanaohitaji huduma na misaada popote walipo kwa usalama na bila masharti yoyote.../