Vikosi vya Yemen vyakaribia kuidhibiti tena Ma’rib
Muungano wa vikosi vya ulinzi vya Yemen umezidisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya waitifaki wa Saudi Arabia na ripoti zinasema jeshi la Yemen linakaribia kuudhibiti tena mji Ma’rib ambao ni makao makuu ya mkoa huo wa kistratijia.
Jeshi na harakati ya kujitolea ya wananchi wa Yemen jana Jumanne walisonga mbele kwa kiasi kikubwa na kukaribia mahali zilipo idara za serikali za mji wa Ma’rib.
Kusonga mbele kwa jeshi na harakati ya kujitolea ya wananchi wa Yemen huko Ma’rib kumewezekana licha ya mashambulizi makubwa ya ndege za kijeshi za Saudia katika mji huo. Shirika la habari la Yemen limeripoti kuwa, jeshi la Yemen na wapiganaji wa kujitolea wa Ansarullah wanakaribia kuudhibiti tena mji huo baada ya kuwarudisha nyuma waitifaki wa Saudi Arabia na magaidi wa mtandao wa al Qaida wanaoungwa mkono na serikali ya Riyadh.
Magaidi hao wanaopewa himaya na Saudia, wamelazimika kuziacha ngome zao kufuatia mashambulizi makali ya jeshi na harakati ya kujitolea ya wananchi wa Yemen.
Habari zinasema kuwa, wapiganaji wa muungano vamizi huko Yemen unaoongozwa na Saudia wamepata hasara kubwa ya kiroho na kimaada katika mapigano hayo. Makamanda wengi wa kijeshi wa adui amma wameuawa au kujeruhiwa katika mapigano na jeshi la Yemen na harakati ya kujitolea ya Ansarullah.
Muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia uliivamia Yemen Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha mdarakani kibaraka wao, Abdu Rabb Mansour Hadi, rais wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbia Saudia.