Iran yaeleza wasiwasi wake kuhusu machafuko na ghasia za Afghanistan
"Afghanistan ya leo imechoshwa na miaka mingi ya kukaliwa kwa mabavu, vita na machafuko, kwa msingi huo makundi yote yanapaswa kujiepusha na machafuko na kuuana wao kwa wao."
Hiyo ni sehemu ya taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa na msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiashiria mapigano yanayoendelea katika eneo la Panjshir huko kaskazini mwa Afghanistan. Saeed Khatibzadeh amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa na mawasiliano na pande zote za Afghanistan na inafanya jitihada kubwa za kupunguza mashaka na masaibu ya Waafghani."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani uingiliaji wa aina yoyote wa kigeni katika masuala ya ndani ya Afghanistan na kusisitiza kuwa, Waafghani wanastahiki kuwa na serikali jumuishi itakayoakisi matabaka na kaumu zote za nchi hiyo.
Ukweli ni kwamba, kuendelea kwa hali tata ya sasa huko Afghanistan kutazidisha hitilafu za ndani na vita na kusababisha madhara makubwa ambayo hayawezi kufidika. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande wake imekuwa ikitangaza kuwa, itafanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu huko Afghanistan na inatarajia kuwa, nchi zote jirani na za kanda hii pia zitaimarisha ushirikiano kwa ajili ya kufikiwa lengo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatulah Ali Khamenei wiki iliyopita alisema katika sehemu moja ya hotuba yake mbele ya baraza jipya la serikali hapa nchini kwamba, Afghanistan ni nchi ndugu ambayo ina lugha, dini na utamaduni sawa na wa Iran. Vilevile alieleza kusikitishwa kwake na matatizo ya watu wa Afghanistan na kusema: "Marekani haijachukua hatua yoyote kwa ajili ya maendeleo ya Afghanistan, na kama Aghanistan ya leo haijarudi nyuma zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 20 iliyopita, basi hapana shaka kwamba haijapiga hatua yoyote ya maana."
Alisema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaliunga mkono taifa madhulumu la Waislamu wa Afghanistan katika hali zote, na uhusiano wa Iran na serikali zingine utategemea mienendo yao na Iran.”
Tehran daima imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba, suala la Aghanistan linapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kushirikisha makabila na kaumu zote za nchi hiyo, kwani mgogoro wa Afghanistan una taathira hasi kwa nchi zote jirani. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, matukio yanayojiri nchini humo yanazidisha wimbi la wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.
Mchambuzi wa masuala ya kistratijia ya kanda ya Magharibi mwa Asia, Abdel Bari Atwan anasema ahadi za Marekani za kurejesha amani, hali bora ya maisha na demokrasia nchini Afghanistan zikuwa hewa na butu kama ilivyokua huko Iraq. Mchambuzi huo amesema, kuna uwezekano wa kutokea vita vya ndani nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa: “Mwenendo wa sasa yumkini ukapelekea kugawanyika nchi ya Afghanistan kwa mujibu wa kaumu na makabila ya nchi hiyo.”
Inatupasa kusema kuwa, Afghanistan ni mhanga wa uingiliaji kati wa madola ya kigeni na uvamizi wa Marekani ambao matunda yake ni uharibifu mkubwa wa miundomsingi, vita na mauaji ya maefu ya raia wasio na hatia. Wakati Marekani ilipoivamia nchi hiyo iliahidi kujenga Aghanistan yenye amani, hali bora ya maisha na demokrasia. Hata hivyo hii leo na baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa kipindi cha miongo miwili na kushiriki katika vita ndefu zaidi katika historia ya Marekani, Washington imeshindwa na kulazimika kuondoka nchini humo kwa fedheha na madhila.
Alaa kulli hal, kwa sasa nchi jirani na Afghanistan zina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya nchi hiyo. Hivyo kuna udharura wa kufanyika jitihada za kutuliza hali ya mambo ya nchi hiyo haraka iwezekanavyo kwa sababu machafuko, vita na mapigano ya ndani vitakuwa na taathira hasi za moja kwa moja kwa nchi zote jirani.
Ni kwa kutilia maanani hayo yote ndipo Iran ikatangaza kwamba, iko tayari kushirikiana na nchi zote zenye nia ya kuimarisha amani na usalama nchini Afghanistan. Pamoja na hayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa, Waafghani wenyewe ndio wanaopaswa kuchukua maamuzi kuhusiana na mustakbali wa nchi yao.