Wapalestina waandamana kwa maelfu kusherehekea metaka 6 waliotoroka jela kishujaa
Maelfu ya Wapalestina katika Ufukwe wa Magharibi na Ukanda wa Gaza wameandamana kwa mnasaba wa kusherehekea kutoroka kishujaa mateka sita Wapalestina waliokuwa wakishikiliwa kwenye jela ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Kwa mnasaba wa ushindi huo adhimu, wanachama na wafuasi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na wa Harakati ya Jihadul-Islami usiku wa kuamkia leo walifanya maandamano katika mji wa Jabaliya ulioko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Akizungumza pembeni ya maandamano hayo, msemaji wa Hamas Abdulatif Qanuu amesema, mateka Wapalestina wameweza kuvivuka vigingi vya ulinzi na kiusalama vya adui na kumshinda adui Mzayuni na vyombo vyake vya usalama.
Miji ya Jenin, al Khalil na baadhi ya maeneo mengine ya Ufukwe wa Magharibi, jana yalikuwa uwanja wa maandamano makubwa yaliyofanywa kwa mnasaba wa kuwa huru mateka sita Wapalestina. Washiriki wa maandamano hayo walitangaza mshikamano wao kwa mateka Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala dhalimu wa Kizayuni.
Zakariya Zubeidi (46), Monadel Yacoub Nafe’at (26), Yaqoub Qassem, Yaqoub Mahmoud Qadri (49), Ayham Nayef Kamamji (35) na Mahmoud Abdullah Ardah (46) ni Wapalestina sita ambao wamefanikiwa kutoroka jela yenye ulinzi mkali zaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya Gilboa kupitia mashimo ya chini kwa chini; na hatua za vyombo vya usalama vya utawala huo haramu za kuwakamata mateka hao hadi sasa zimegonga mwamba.../