Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu hali hatari ya Ukanda wa Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i745-umoja_wa_mataifa_watahadharisha_kuhusu_hali_hatari_ya_ukanda_wa_ghaza
Ripoti mbalimbali kuhusu Ghaza zinabainisha kuwa eneo hilo linakabiliwa na hali mbaya kutokana na kusuasua zoezi la kukarabati uharibifu uliosababishwa na jinai kubwa za utawala wa Kizayuni hususan katika vita vitatu vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 07, 2016 00:11 UTC
  • Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu hali hatari ya Ukanda wa Ghaza

Ripoti mbalimbali kuhusu Ghaza zinabainisha kuwa eneo hilo linakabiliwa na hali mbaya kutokana na kusuasua zoezi la kukarabati uharibifu uliosababishwa na jinai kubwa za utawala wa Kizayuni hususan katika vita vitatu vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza.

Hali mbaya ya Ghaza inahitajia kuchukuliwa hatua za haraka na kubwa kimataifa ili kutatua hali inayolikabili eneo hilo lililo chini ya mzingiro na lililoathiriwa na vita. Robert Piper Naibu Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Mwenendo wa Amani wa Mashariki ya Kati na ambaye pia ni Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu kwa ajili ya Palestina amesema hali ya mambo ya Ghaza ni ya hatari. Akiwa katika ziara yake huko Ghaza, Robert Piper amesema kuwa mafanikio yamepatikana, hata hivyo hatua hizo hazitoshi kwa ajili ya kulijenga upya eneo hilo na kwamba Ghaza iko katika hatari. Amesema kuwa eneo la Ukanda wa Ghaza linakabiliwa na hali mbaya ya mambo huku utawala wa Kizayuni ukizuia kikamilifu kuingizwa katika eneo hilo vifaa vya ujenzi na hivyo kuifanya hali ya kiuchumi ya Ghaza kulegalega pakubwa. Amesema, kwa msingi huo Umoja wa Mataifa kwa dhati unaiomba jamii ya kimataifa kuwasaidia wananchi wa Ghaza. Robert Piper ameyasema hayo huku hali ya wasiwasi ikiongezeka kila uchao kutokana na uwezekano wa kuzuka vita vipya huko Ghaza. Utawala wa Kizayuni ambao kwa kushadidisha mzingiro wa kiuchumi huko Ghaza katika kipindi cha miaka minane iliyopita, umewasababishia raia wa Kipalestina wa eneo hilo matatizo chungu nzima. Katika miaka ya hivi karibuni mbali na kuuzingira Ukanda wa Ghaza, utawala huo umeanzisha pia vita vitatu dhidi ya wakazi wa eneo hilo wasio na hatia. Ukanda wa Ghaza tangu mwishoni mwa mwaka 2008 umeshuhudia vita vitatu vya umwagaji damu vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya wakazi wa Kipalestina eneo hilo; na katika vita vya mwisho yaani vita vya siku 50 vilivyoanzishwa na Israel mwaka 2014, Wapalestina zaidi ya 2000 wasio na hatia, waliuliwa shahidi. Kuhusiana na suala hilo, Shirika la Misaada la Kimataifa (Oxfam) ambalo linayashirikisha mashirika na taasisi za kujitolea za kimataifa 30, limetahadharisha kuhusu athari zinazowezwa kusababishwa na hali mbaya ya mambo ya Ghaza na kutoondolewa mzingiro katika ukanda huo. Oxfam imetangaza kuwa iwapo mzingiro wa kiuchumi wa Israel hautaondolewa na mazingira ya kuruhusu kuingizwa vifaa na zana za ujenzi huko Ghaza hayataandaliwa, basi kazi ya ujenzi mpya wa eneo hilo lililoathiriwa na vita vya hivi karibuni vya utawala wa Kizayuni itachukua makumi ya miaka. Utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ulianzisha vita hivyo dhidi ya Ghaza tarehe nane mwezi Julai mwaka juzi na kusimamisha mashambulizi yake hayo tarehe 26 mwezi Agosti kufuatia makubaliano ya kusimamisha vita iliyofikia na makundi ya Kipalestina kwa upatanishi wa Misri huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo, haukufikia hata lengo lake moja la kuanzisha vita hivyo. Aidha umekataa kuheshimu makubaliano hayo kwani katika muda huu wote, utawala wa Kizayuni si tu haujapunguza kulizingira eneo la Ghaza, bali umeshadidisha kabisa mzingiro huo; huku kila uchao ukizidisha vitendo vyake vya kidhulma na ukandamizaji dhidi ya raia wa Kipalestina. Hii ni katika hali ambayo serikali za Ulaya zilizoahidi kutoa misaada ya ujenzi mpya wa Ghaza pia zimesema kuwa, kutolewa msaada wowote kwa ajili ya Ghaza kutategemea na kudhaminiwa usalama Israel na ikiwa na maana ya kukwepa kikamilifu ahadi walizotoa kwa ajili ya ujenzi mpya wa Ghaza. Kiujumla ni kuwa, kuendelea kutolewa radiamali kimataifa katika mwaka huu wa 2016 dhidi ya jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni kunaashiria kushindwa utawala huo kuficha jinai zake; na hatua hiyo inaonyesha kuwa jinai za kutisha za utawala wa Israel kamwe haziwezi kufutika katika fikra za watu.