Mpango wa Chakula watahadharisha kuhusu kuongezeka njaa nchini Afghanistan
Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetahadharisha kuhusiana na kuongezeka baa la njaa nchini Afghanistan.
Taarifa iliyotolewa na shirika hilo la kimataifa imeeleza kuwa, takribani familia zote za Waafghani hivi sasa zinataabika kwa njaa na uhaba mkubwa wa chakula.
Sehemu moja ya taarifa ya Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) inaeleza kuwa, uhaba wa chakula nchini Afghanistan umekuwa mkubwa kiasi kwamba, baadhi ya familia zimelazimika kupungua milo yao kwa siku.
Baadhi ya ripoti zinasema, baadhi ya familia zinalazimika kuwapa chakula watoto tu huku watu wazima katika familia wakilazimika kubakia na njaa kutokana na kutokuweko chakula cha kutosha.
Ripoti hiyo ya WFP inatolewa siku moja tu baada ya Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa, asilimia 97 ya wananchi wa Afghanistan wamo katika hatari ya kuingia katika maisha ya chini ya mstari wa umasikini.
Hivi karibuni pia, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu, (OCHA) ilitangaza kuwa, mamilioni ya wananchi wa Afghanistan wanahitajia misaada ya chakula pamoja na huduma za kiafya na kwamba, kwa sasa sekta ya utoaji huduma nchini Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya na imo katika hatua ya kusambaratika.
Afghanistan ambayo ni moja kati ya nchi masikini zaidi duniani hivi sasa inakabiliwa na hali mbaya zaidi kutokana na kuzorota uchumi wa nchi hiyo.