Umoja wa Kiarabu washirikiana na utawala wa Kizayuni kuituhumu Iran
Katika siku za karibuni, Marekani kwa mara nyingine imeamua kushirikiana na washirika wake wa Mashariki ya Kati katika kutilia shaka mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani na kuutaja kuwa ni tishio kwa usalama wa eneo.
Katika kikao chake cha karibuni, kamati ya Umoja wa nchi za Kiarabu ilitoa taarifa iliyojaa uongo, tuhuma na uzushi na bila kuashiria silaha za nyuklia za utawala wa kigaidi wa Israel, ikadai kwamba mpango wa nyuklia wa Iran ni tishio kwa usalama wa Asia Magharibi. Huku wakiwa wanafuatilia malengo maalumu, waandaaji wa taarifa hiyo wametaka kuanzishwa mkakati maalumu kwa ajili ya kuchunguza haraka iwezekanavyo vituo vyote vya nyuklia vya Iran.
Sambamba na tuhuma hizo, Yair Lapid, Waziri wa Mambo ya Nje wa utawala wa Israel akiwa safarini mjini Moscow amedai kwamba Iran inafanya juhudi za kuunda silaha za nyuklia. Akizungumza Ijumaa na shirika la habari la Sputnik, Yair Lapid amedai kwamba Iran inakaribia kuunda silaha za nyuklia. Akizungumza mapema Alkhamisi akiwa na waziri mwenzake wa Russia, Sargey Lavrov, Lapid alitumia lugha ya vitisho dhidi ya Iran na kudai kuwa nchi hii imeazimia kutengeneza silaha za nyuklia.
Matamshi ya viongozi wa sasa wa utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Iran kwa hakika ni ya kuchekesha na yanalenga kupotosha fikra za waliowengi duniani kuhusiana na siasa zao halisi za kukandamiza taifa la Palestina na kuendelea kuficha silaha zao za nyuklia ambazo zinahatarisha usalama wa eneo zima la Asia Magharibi. Matamshi hayo ya kichekesho dhidi ya Iran kwa hakika yanafanana na yale yaliyotolewa huko nyuma na Benjamin Netanyahu waziri mkuu wa zamani wa utawala huo katika Baraza la Usalama na kupuuzwa na dunia nzima kwa kuwa hayakuwa na ukweli wala msingi wowote.
Siasa za kuidhihirisha Iran kuwa 'tishio kwa usalama' ni sehemu ya harakati za kichochezi ambazo zimekuwa zikienezwa kwa muda mrefu sasa na Marekani, utawala wa Israel na vibaraka wao wa Kiarabu katika eneo.
Katika barua aliyomwandikia mkuu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na vitisho vya mara kwa mara vya watawala wa Israel dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya kiraia, Zahra Irshadi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika umoja huo alitahadharisha dhidi ya hatua yoyote ya kipumbavu na chockochoko zinazoweza kufanywa na utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran na kusema Jamhuri ya Kiislamu kwa mujibu wa haki yake ya wazi na iliyosimamama juu ya msingi wa sheria za kimataifa, inayo haki ya kulinda raia, maslahi, taasisi na utawala wake dhidi ya kila aina ya hatua za kigaidi na uharibifu.
Swali ni kwamba je, ni kweli kuwa utawala wa Kizayuni na baadhi ya tawala vibaraka za Kiarabu ambazo tayari zimeanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia na utawala huo ghasibu na wa kigaidi zina wasiwasi kweli kuhusu usalama wa eneo? Bila shaka jibu la swali hili ni hapana.
Ni wazi kuwa uchochezi unaofanywa na tawala hizo unafuatilia malengo maalumu ambapo moja ya malengo hayo ni kuweka pembeni suala zima la Palestina na kufunika sababu za migogoro na vita vinavyoibuliwa mara kwa mara katika eneo kwa ushirikiano wa Marekani, Israel na Saudi Arabia.
Gareth Porter, Mchambuzi mashuhuri wa Marekani anasema:
Ukweli wa mambo ni kuwa chanzo kikuu cha tishio la usalama katika eneo la Asia Magharibi ni nchi ambazo zitumia nguvu zao zote kununua silaha na zana za kivita kutoka Marekani.
Ni wazi kuwa Israel na tawala za Kiarabu ambazo zimesaliti malengo ya taifa la Palestina ndicho chanzo cha matatizo yote ya usalama katika eneo. Ushirikiano wa tawala vibaraka za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel katika kukariri madai yasiyo na msingi kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni tishio kwa usalama wa eneo kwa hakika ni aina fulani ya kutaka kuuhadaa ulimwengu kuhusu suala hilo. Israel inatoa vitisho dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani katika hali ambayo mpango huo unasimamiwa kikamilifu na Wakala wa Kiamataifa wa Nishati ya Nyuklia IAEA. Hii ni katika hali ambayo utawala huo ambao hauruhusu wakaguzi wa wakala huo kukagua magahala yake ya silaha za nyuklia, una kati ya vichwa 200 hadi 300 vya silaha hizo angamizi dhidi ya jamii ya mwanadamu.
Kama alivyosema Saeed Khatibazadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika kujibu vitisho hivyo vya Israel, bila shaka taarifa kama hizo zinauhudumia wazi na kisiri utawala ghasibu wa Israel.