Mbunge: Waueni mateka wote wa Kipalestina ili wasiweze kutoroka tena
Mbunge mmoja wa Bunge la utawala wa Kizayuni wa Israel mwenye misimamo mikali na chuki za kupindukia dhidi ya Wapalestina ametoa wito wa kuuawa kwa kunyongwa mateka wote wa Palestina ili wasiweze kutoroka tena kutoka gerezani.
Itamar Ben Ghafir, amevitaka vyombo husika huko Israel kuwanyonga mateka wote wa Kipalestina akibainisha kwamba, mateka ambaye ni mfu hatoweza kutoroka kutoka gerezani.
Akizungumzia sakata la kutoroka mateka wa Kipalestina kutoka gerezani, Mbunge huyo mwenye chuki na Wapalestina amesema: Navipongeza vikosi vya usalama kwa kufanikiwa kuwakamata mateka wanne kati ya sita waliotoroka kutoka jela, lakini nashangazwa mno kwa nini vikosi vya usalama havijawaua Wapalestina hao, tulipaswa kuwaua.
Wakati huo huo, makundi ya muqawama huko Palestina yameonya kwamba, kama mateka wa Kipalestina wanaosakwa na Israel wataingia katika mji wa Jenin basi watawalinda na kuwatetea kwa damu na roho zao.
Alfajiri ya Jumatatu iliyopita mateka watano wa Kipalestina wanachama wa harakati ya Jihad Islami na mmoja na harakati ya Fat-h ambao walihukumiwa kifungo cha muda mrefu walifanikiwa kutoroka jela ya Gilboa yenye ulinzi mkali huko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu ambayo ni moja kati ya jela kuu za kiusalama za utawala haramu za Israel. Wapalestina wanne kati ya sita kwa mujibu wa duru za Israel wameshatiwa mbaroni.