Maelfu ya Wayemen waandamana nchini Marekani kulaani jinai za Saudia
Maelfu ya Wayemen wamefanya maandamano katika miji ya New York, Michigan na California kulaani mauaji ya Abdul Malik al Sanabani (30), mwanachuo mwenye asili ya Yemen aliyekuwa akiishi nchini Marekani.
Televisheni ya Al Masirah imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, washiriki wa maandamano hayo wamelaani vikali jinai iliyofanywa na mamluki wa madola vamizi ya Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ya kumpora, kumtesa na hatimaye kumuua mwanafunzi huyo wa chuo kikuu aliyekuwa anaelekea mjini Sana'a.
Ripoti hiyo vile vile imesema kuwa, waandamanaji wametaka kuondolewa mzingiro wa Yemen na kufunguliwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sana'a ili kuwapunguzia masaibu wananchi maskini na wasio na ulinzi wa Yemen. Wanasiasa mbalimbali wa Marekani nao wameshiriki kwenye maandamano hayo.
Baraza la Uratibu wa Wageni na Taasisi la nchini Uingereza nalo limelaani vikali jinai hiyo na kutaka kupandishwa kizimbani wahalifu wote waliofanya mauaji na jinai hiyo.
Mauaji ya kikatili aliyofanyiwa Abdul Malik al Sanabani, kijana wa Yemen aliyekuwa masomoni nchini Marekani yanaendelea kulaaniwa vikali. Jinai hiyo imetokea kwenye mkoa wa Lahj wa mashariki mwa Sana'a, mji mkuu wa Yemen. Mamluki wa Saudi Arabia na Imarati walimsimamisha kijana huyo katika kituo kimoja cha upekuzi kwenye wilaya ya Tour Al-Baha mkoani Lahj.
Kutokana na wavamizi wa Yemen hasa Saudia na Imarati kupiga marufuku kutua ndege katika uwanja wa kimataifa wa Sana'a, al Sanabani alilazimika kushuka ndege katika uwanja wa Aden wa kusini mwa Yemen na kuamua kusafiri kwa gari kuelekea Sana'a, lakini wahalifu ambao ni mamluki wa Saudia na Imarati walimsimamisha njiani, wakamshambulia, wakampora vitu vyake na baadaye kumuua kikatili na kidhulma.
Kosa pekee lililopelekea kijana huyo Myemen kuuliwa kikatili na kidhulma na mamluki wa Saudi Arabia na Imarati ni kumiliki kwake fedha za kigeni, kukodi taxi na kujipiga picha yaani selfie.