Saudi Arabia ndiyo inayoongoza ukandamizaji wa raia wa kusini mwa Yemen
Huku maandamano ya wananchi wa kusini ya Yemen yakipamba moto dhidi ya wavamizi wa nchi yao, harakati moja ya nchi hiyo imesema kuwa, Saudi Arabia ndiyo inayoongoza ukandamizaji wanaofanyiwa waandamanaji hao.
Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, mikoa ya kusini mwa Yemen ambayo iko chini ya udhibiti wa mamluki wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) imekumbwa na maandamano makubwa ya wananchi wanaolalamikia hali mbaya ya maisha, kuporomoka thamani ya safaru ya taifa, kuzimwa muda mrefu umeme na huduma sifuri zinazotolewa na wanaoshikilia mikoa hiyo.
Waandamanaji hao wanataka kupinduliwa mamluki wa Saudia na Imarati kusini mwa Yemen. Hata hivyo mamluki hao wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi kukandamiza maandamano ya wananchi hao ambapo habari ya karibu inasema kuwa mtu mmoja ameuliwa kwa kupigwa risasi na mamluki hao na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Maandamano yanaendelea katika mikoa ya kusini mwa Yemen ikiwemo Aden na kumezuka pia mapigano ya silaha baina ya mamluki wa Saudia na Imarati, suala ambalo lilimpelekea mkuu wa baraza la mpito la kusini kutangaza hali ya hatari na marufuku ya kutotoka nje katika mikoa yote ya kusini mwa Yemen.
Baraza hilo ni la mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) ambayo ni moja ya wavamizi wakuu wa nchi ya Kiislamu ya Yemen. Baraza hilo liliundwa mwaka 2017 na hivi sasa linadhibiti mkoa wa Aden. Linadhibiti pia mkoa wa Socotra wa kusini mashariki mwa Yemen na baadhi ya maeneo mengine ya kusini mwa nchi hiyo.