Syria: Tunakaribisha ushirikiano wowote baina ya Iran na nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i75116-syria_tunakaribisha_ushirikiano_wowote_baina_ya_iran_na_nchi_za_kiarabu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amezungumzia msimamo wa nchi yake wa kukaribisha ushirikiano wa aina yoyote baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Kiarabu na kusisitiza kuwa, Damascus haitishwi kivyovyote na majigambo ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 27, 2021 04:02 UTC
  • Syria: Tunakaribisha ushirikiano wowote baina ya Iran na nchi za Kiarabu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amezungumzia msimamo wa nchi yake wa kukaribisha ushirikiano wa aina yoyote baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Kiarabu na kusisitiza kuwa, Damascus haitishwi kivyovyote na majigambo ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Televisheni ya al Mayadeen imemnukuu Faisal Mekdad  akisema hayo jana na kuongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazihami nchi za Kiarabu na muda wote imekuwa pamoja na wananchi wa Syria na Palestina hivyo kuna wajibu wa kupokea kwa njia nzuri nia njema na vitendo vizuri vya Iran.

Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Mekdad amekosoa vikali misimamo ya nyuso mbili ya nchi za Magharibi kuhusu serikali na wananchi wa Syria na kusisitiza kuwa, nchi yake haiziamini hata kidogo nchi za Magharibi. Nchi hizo zimemimina na kupandikiza magenge ya kigaidi ndani ya ardhi ya Syria na hadi hivi sasa zinaendelea kuyaunga mkono na kuyasaidia kwa hali na mali magenge hayo ya makatili na wauaji wa wananchi wa Syria.

 

Amesema, wakati linapofika suala la kuwasaidia na kuwahami ndugu zetu wa Lebanon, sisi hatuuogopi utawala wa Kizayuni wala dola jingine lolote.

Ikumbukwe kuwa tarehe 11 Disemba 2019, Congress ya Marekani iliiwekea vikwazo Syria ambapo awamu ya kwanza ya vikwazo hivyo ilianza kutekelezwa tarehe 17 Julai mwaka huu. Lengo la vikwazo hivyo ni kukwamisha juhudi za kuijenga upya Syria baada ya kuharibiwa vibaya na magenge ya kigaidi yaliyoingizwa nchini humo na madola hayo hayo ya kibeberu ya Magharibi yaani nchi za Ulaya na Marekani.