Mamluki wa Imarati wazidi kutwangana wenyewe kwa wenyewe Yemen
Duru za habari zimetangaza kuwa, makundi mawili ya mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) yanatwangana vibaya katika mkoa wa Aden, wa kusini mwa Yemen, na kupelekea watu kuuawa na wengine kujeruhiwa.
Shirika la habari la Reuters, kitengo cha lugha ya Kiarabu limenukuu baadhi ya duru za kiusalama zikithibitisha habari hiyo na kusema kuwa, mapigano makali baina ya mamluki wa Imarati yalitokea jana (Jumamosi) asubuhi katika eneo la Crater mkoani Aden, kusini mwa Yemen.
Kwa mujibu wa shirika hilo la Reuters, mapigano hayo yametokea baina ya "vikosi vya ukanda wa usalama" na jeshi la polisi la Baraza la Mpito la Kusini, makundi ambayo yote ni ya mamluki wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati). Watu wanne wameuawa na wengine kujeruhiwa kwenye mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe.
Kwa mujibu wa shirika hilo, vikosi vya ukanda wa usalama vimeshambulia maeneo kadhaa ya makazi ya raia na kusababisha hasara katika vituo kadhaa vya biashara na nyumba za raia.
Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Aden imetoa taarifa na kuwataka wakazi wa eneo la Crater wabakie majumbani mwao hadi pale operesheni ya kuwasafisha magaidi itakapokamilika.
Kwa muda mrefu mkoa wa Aden unashuhudia mapigano baina ya mamluki wa Saudi Arabia yaani serikali ya mkimbizi Abdu Rabuh Mansour Hadi na Baraza la Mpito la Kusini ambalo ni la vibaraka na mamluki wa Imarati. Sasa hivi lakini mapigano yametokea baina ya mamluki wa Imarati wenyewe kwa wenyewe.