Kutiwa kiwewe utawala wa Bahrain na maandamano ya wananchi
Hivi karibuni akthari ya miji ya Bahrain ilishuhudia maandamano makubwa ya wananchi wa nchi hiyo ya kupinga safari ya Yair Lapid, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala haramu wa Israel katika nchi yao.
Yair Lapid aliwasili Manama mji mkuu wa Bahrain Alkhamisi iliyopita ikiwa ni katika fremu ya utekelezaji wa makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu yaliyofikiwa Septemba mwaka jana (2020). Moja ya malengo ya safari ya Yair Lapid yalikuwa ni kufunguliwa ubalozi wa utawala haramu wa Israel mjini Manama. Katika kulalamikia safari hiyo, wananchi wa Bahrain walifanya maandamano makubwa wakisisitiza kwa mara nyingine tena kuwa, katu hawatavumilia na kuridhia suala la nchi yao kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.
Mbali na kuchoma moto bendera ya utawala wa Kizayuni na matairi ya magari, waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na maberamu ya kupinga utawala wa Aal Khalifa walipaza sauti zao pia kutoa nara za kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel.
Watumiaji mitandao ya kijamii nchini Bahrain nao pia wameendesha kampeni maalumu ikiwa na hashtagi za kupinga Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala wa Kizayuni kuingia katika ardhi ya nchi yao.
Wananchi wa Bahrain wanaitaja hatua ya utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala khabithi wa Israel kuwa ni doa jeusi kwa taifa lao. Maandamano ya wananchi hao ya kulalamikia safari ya mgeni asiyetarajiwa katika nchi yao yalikabiliwa na ukandamizaji wa vikosi vya usalama huku jamii ya kimataifa ikiendelea kutia pamba masikioni na kufumbia macho ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika nchini Bahrain.
Kuendelea kushuhudiwa maandamano makubwa nchini Bahrain ni ishara ya wazi ya kuweko mgawanyiko mkubwa baina ya watawala na wananchi wa nchi hiyo. Ukweli mwingine unaodhihirika shahir shahir katika matukio ya Bahrain ni kwamba, utawala wa nchi huyo haujaingia madarakani kwa ridhaa ya wananchi na hata kipaumbele cha viongozi hao kuhusiana na matukio ya ulimwengu ni tofauti na matakwa ya wananchi. Ushahidi wa wazi ni upinzani mkubwa wa wananchi wa Bahrain kwa safari ya Yair Lapid, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala haramu wa Israel katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Upinzani na maandamano ya wananchi umezidi kuutia kiwewe na hofu utawala wa Aal Khalifa hasa kutokana na kuwa, umediriki kwamba, hauna uhalali mbele ya wananchi na haukubaliki. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana hivi sasa utawala wa Bahrain unatafuta uhalali nje ya mipaka ya nchi hiyo na kuufanya utawala haramu wa Israel kama tegemeo lake la kuhalalisha mamlaka na ushikaji hatamu wake nchini Bahrain. Hata hivyo watawala wa Manama wameghafilika na ukweli huu kwamba, hata utawala dhalimu wa Israel nao hauna uhalali na kwamba, wenyewe pia unatafuta kuhalalisha uwepo wake.
Moja ya wasiwasi na sababu kuu ya wahaka na hofu ya utawala wa Aal Khalifa ni suala la ukiukaji wa haki za binadamu ambao imeufanya dhidi ya wananchi wake. Kuhusiana na hilo, hivi karibuni Kanali ya Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar ilifichua katika ripoti yake kwamba, katika kipindi cha kati ya mwaka 2011 hadi 2021, utawala wa Bahrain umewafunga jela takribani watoto 607 na umekuwa ukiwafanyia mateso ya aina mbalimbali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto hao wamekuwa wakifanyiwa usaili bila ya kuweko familia zao na mawakili wao. Kwa muktadha huo, Bahrain ina wasiwasi wa ndani na wa nje wa kufanyika uchunguzi wa asasi huru kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo, na ni kutokana na sababu hiyo ndio maana umeamua kuukimbilia utawala haramu wa Israel na kuamua kuanzisha nao uhusiano wa kawaida. Hata hivyo watawala wa Manama wameghafilika kabisa kwamba, Israel siyo tu kwamba, haiwezi kuwa kinga na kizuizi cha kusambaratika utawala wao bali hatua yao hiyo ya kujikurubisha kwa Tel Aviv itaharakisha mwenendo wa kusambaratika utawala wao. Hii ni kutokana na kuwa, maandamano ya wananchi wa Bahrain yaliyoanza Alkhamisi iliyopita sambamba na safari ya Yair Lapid Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala haramu wa Israel yameongezea wasiwasi na wahaka mkubwa viongozi wa Manama.
Katika upande mwingine, makundi ya mapambano ya Palestina sambamba na kulaani hatua ya Bahrain ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala vamizi wa Israel yameitaja hatua hiyo kuwa ni khiyana na usaliti kwa malengo matukufu ya Palestina.
Taarifa ya pamoja ya makundi ya Palestina katika Ukanda wa Gaza imeeleza kuwa, safari ya Yair Lapid huko Bahrain na kufunguliwa ubalozi wa Israel katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu ni kuusaliti Uislamu, jamii ya Waarabu na wananchi wa Palestina na Bahrain.
Kwa msingi huo basi, kuna dhana hii kwamba, katika siku za usoni na miezi ijayo, kutashuhudiwa kuongezeka mashinikizo ya ndani, kieneo na kimataifa dhidi ya utawala wa Aal Khalifa; na utawala huo hautapata faida yoyote ya maana ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel ghairi ya kusambaratika.