Jihad Islami: Ukingo wa Magharibi utakuwa makaburi ya ndoto za Wazayuni
-
Khalid al Batsh
Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetangaza kuwa, hatua ya kuzuia Gaza kuwa na nafasi muhimu katika mpango wa kitaifa wa Palestina itafeli na kushindwa na kwamba eneo la Ukingo wa Maghariibi litakuwa makaburi ya njama na ndoto za Wazayuni wa Israel.
Khalid al Batsh ambaye ni mjumbe wa ngazi za juu wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema kuwa damu ya mashahidi wa Ukingo wa Magharibi na wa Quds imechanganyika na kwamba kuchanganyika kwa damu hiyo ni kielelezo cha mtazamo sahihi wa udharura wa kukombolewa Palestina na kurejea wakimbizi katika ardhi na makazi yao yaliyovamiwa na walowezi wa Kizayuni.
Al Batsh amesema kuwa, Quds ndiyo itakayokuwa chachu ya vita dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa, matokeo muhimu zaidi ya vita vya Panga la Quds huko Ghaza ni msisitizo wa kuwepo mshikamano wa taifa la Palestina huko Quds, Ukingo wa Magharibi na ardhi zote za Palestina zilizoghusubiwa mwaka 1848.
Afisa huyo wa harakati ya Jihad Islami ametahadharisha kuhusu kuendelezwa mzingiro wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, suala hilo litasababisha mlipuko mkubwa.
Vilevile amelaani mwenendo wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuwataka Wapalestina waendeleze mapambano yao hadi watakapofanikiwa kukomboa nchi yao.