Jeshi la Yemen latungua droni ya Saudia mkoani Ma'rib
Jeshi la Yemen limetangaza habari ya kutungua ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya Saudi Arabia wakati ikiwa katika oparesheni ya kijasusi katika mkoa wa Ma'rib, katikati mwa nchi.
Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree amesema hayo leo Jumatano na kuongeza kuwa, ndege hiyo isiyo na rubani ya muungano wa kivita wa Saudia aina ya CH-4 iliyotengenezewa China imetunguliwa na vikosi vya Yemen alfajiri ya leo katika mkoa wa Ma'rib.
Brigedia Jenerali Saree ameongeza kuwa, droni hiyo imetunguliwa ikiwa katika oparesheni za kiadui katika anga ya wilaya ya al-Jubah katika mkoa wa Ma'rib.
Amesema ndege hiyo ya kijasusi isiyo na rubani imetunguliwa kwa kutumia kombora la ardhini hadi angani la kikosi cha ulinzi wa anga cha jeshi la Yemen.
Jeshi la Yemen mara kwa mara limekuwa likitungua ndege zisizo na rubani za Saudia na Marekani katika anga ya nchi hiyo ya Kiarabu inayozongwa na vita tokea Machi 2015.