Majasusi wa Israel wahukumiwa kifo Ukanda wa Gaza
Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti kuwa, Mahakama ya Kijeshi ya Ukanda wa Gaza imewahukumu kifo majajusi sita wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mahakama ya Kijeshi ya Ukanda wa Gaza imetangaza leo kwamba, hukumu hizo za vifo dhidi ya majajusi sita wa utawala ghasibu wa Israel zilitolewa mwezi Septemba na mwezi huu wa Oktoba na kwamba majasusi wenne wa utawala huo wamehukumiwa adhabu ya kazi ngumu hadi kifungo cha maisha jela. Mtuhumiwa mmoja kati ya majasusi wa Israel hakupatikana na hatia.
Taarifa iliyotolewa na Mahakama ya Kijeshi ya Gaza imesema: hukumu hizo zimetolewa katika utekelezaji wa majukumu ya mahakama ya kulinda jamii ya Wapalestina mkabala wa majasusi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Imeongeza kuwa, kwa mujibu wa sheria za mahakama zilizopasishwa mwaka 19079, hukumu zote zilizotolewa zimepitia awamu zote zilizoainishwa.
Mahakama ya Kijeshi ya Ukanda wa Gaza imesisitiza kuwa, majasusi wa Israel watakaojisalimisha wenyewe kwa vyombo vya sheria watafaidika na tahfifu katika hukumu zao.
Miezi saba iliyopita pia Mahakama ya Kijeshi ya Ukanda wa Gaza ilimhukumu kifo jasusi mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuvujisha taarifa kwa vyombo vya ujasusi vya adui.