May 24, 2016 05:58 UTC
  • Matukio ya hivi karibuni ya Syria kufuatia kuzidi kupata pigo magaidi

Waziri wa Habari wa Syria amesema kuwa, miripuko ya siku za hivi karibuni ikiwemo ile iliyotokea jana magharibi mwa nchi hiyo ni ishara ya wazi kuwa magaidi wameshindwa katika medani za mapambano.

Omran al Zoubi jana alilaani vikali miripuko ya mabomu iliyotokea katika mkoa wa Latakia wa magharibi mwa Syria na kusema kuwa, yaliyofanya jinai hizo ni makundi ya kigaidi ambayo yameshindwa kukabiliana na jeshi la serikali katika medani za mapambano. Waziri wa Habari wa Syria amesisitiza kuwa, magenge ya kigaidi yamepata pigo kubwa katika medani ya mapambano na hivyo yameamua kumalizia hasira zao kwa kuua watu wasio na hatia. Al Zoubi ameongeza kuwa, Damascus haitoruhusu damu za watu wasio na hatia zimwagwe vivi hivi na magaidi. Ikumbukwe kuwa jana Jumatatu kulitokea miripuko mikubwa katika miji ya bandari ya Jableh na Tartus katika viunga vya Latakia, magharibi mwa Syria na kupelekea zaidi ya raia 100 wa kawaida wa nchi hiyo kuuawa na wengine zaidi ya 120 kujeruhiwa. Hii ni katika hali ambayo magenge ya kigaidi yanazidi kupata vipigo katika maeneo tofauti ya Syria, huku kitali kikishadidi baina ya magenge hayo ya kitakfiri, yenyewe kwa yenyewe. Si hayo tu, lakini waasi zaidi wanazidi kujisalimisha kwa jeshi la serikali. Habari za hivi karibuni kabisa zinasema kuwa, waasi 155 wameweka silaha chini na kujisalimisha kwa serikali katika mji wa Homs wa katikati mwa Syria na kutangaza kuwa wanajuta kujiunga na magenge ya kigaidi. Tarehe 8 mwezi huu wa Mei pia, waasi 210 waliweka chini silaha na kujisalimisha kwa serikali katika kitongoji kimoja cha viwanda mkoani Homs na kuahidi kuwa hawatotenda tena vitendo vya kigaidi. Fauka ya hayo mapigano na mizozo imeongezeka kati ya magenge ya kigaidi yenyewe kwa yenyewe, kutokana na magaidi hao kuzidi kupoteza maeneo waliyokuwa wanayashikilia. Ugomvi mkubwa kati ya magenge hayo ni kila moja kutaka kuwa na eneo kubwa zaidi linalolidhibiti. Genge la kigaidi lijulikanalo kwa jina la Jayshul Islam na magenge mengine 23 yamekuwa yakilaumiana kuhusu kuzuka vita baina yao katika viunga vya Damascus jambo ambalo linazidi kutoa pigo kwa magenge hayo ya kitakfiri. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, idadi ya wanamgambo walioangamizana wenyewe kwa wenyewe katika vita vya ndani imepindukia elfu moja. Mbali na hayo, zaidi ya wanamgambo 1500 wa pande hizo hasimu wametekwa na mamia ya raia wa kawaida wa Syria wanaoishi kwenye maeneo hayo imma wameuawa au kujeruhiwa. Kufuatia kushadidi kitali baina ya magenge ya kitakfiri, kundi la Jayshul Islam na makundi mengine 23 ya kigaidi yameyaonya magenge mengine ya kitakfiri yaliyojiunga na Jabhatun Nusra kwamba imma yakubaliane na makubaliano mapya ya kusimamisha mapigano baina yao tena bila ya masharti yoyote, au yajikubalishe kukumbwa na mashambulizi makali katika kipindi cha masaa 24 yajayo. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, magenge ya kigaidi yanayopata uungaji mkono wa madola ya kigeni huko Syria, hayana nia njema kwa taifa na wala kwa wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu, bali kitu pekee yanachozingatia ni maslahi yao binafsi.

Tags